2014-03-29 08:19:24

Mkutano mkuu wa Maaskofu Katoliki Italia kufunguliwa na Papa Francisko, Mei, 2014


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, utakaoadhimishwa mwezi Mei mwaka huu. Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kumteua Askofu Nunzio Galantino kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kipindi cha miaka mitano na kwamba, atakuwa ni chombo muhimu kitakachowaunganisha Maaskofu katika kudumisha na kukoleza udugu, ushiriki, usikilizaji na majadiliano ya kweli na uwazi kati ya Maaskofu.

Hii ni sehemu ya tamko kutoka Kamati kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia baada ya kuhitimisha kikao chake hivi karibuni hapa mjini Roma. Maaskofu wamekazia umuhimu wa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa wale wasiokuwa na fursa za ajira; athari zinazotokana na myumbo wa uchumi kimataifa ambao umepelekea familia nyingi kujikuta zinakabiliana na hali ngumu ya maisha na mpasuko katika maisha ya ndoa na familia. Wananchi wengi wa Italia kwa sasa wanaelemewa na umaskini wa hali na kipato; umaskini wa maadili, utu wema na maisha ya kiroho. Makundi yote haya hayana budi kusaidiwa kikamilifu katika safari ya maisha yao ya kiutu na kiroho.

Kamati kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limejadili kwa kina na mapana jinsi ya kupambana na mmong'onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema; rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; sera za kisiasa zinazokwenda kinyume na ubinadamu. Kuna haja wanasema Maaskofu kuvuka vikwazo vinavyokwamisha maisha ya ndoa na familia; uhuru wa wazazi na walezi kuchagua mfumo wa elimu wanaoupenda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, kwa kuwasaidia wale walioathirika wakiwa njiani kuelekea Yeriko kutoka na ubinafsi wa kutupwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mkutano wake, limekazia umuhimu wa Shule za Kikatoliki na mchango wake katika ustawi na maendeleo ya wengi. Wamejadili pia kuhusu maisha ya kitawa kwa kuangalia mambo msingi na taratibu zinazoweza kutumiwa na Kanisa Katoliki nchini Italia. Wamefanya tafakari ya kina kuhusu Hati ya Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Juma la Kijamii nchini Italia na kuridhika kuhusiana na mwelekeo na katekesi yake na kwamba, hati hii itajadiliwa wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, utakaofanyika mwezi Mei, 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.