2014-03-29 11:29:18

Mashambulizi ya Boko Haram yanachafua uhusiano kati ya Waislam na Wakristo!


Nigeria ni nchi ambayo ina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo Barani Afrika, mahali ambapo waamini wa dini hizi mbili, wanaishi katika amani na utulivu pamoja na kuendelea kuwathamini waamini wa dini za jadi Barani Afrika. Kwa bahati mbaya katika miaka ya hivi karibuni kumejitokeza watu wenye misimamo mikali ya kidini inayojikita pia katika vitendo vya kigaidi kama inavyojionesha kwa kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria kinachovuruga amani na utulivu nchini Nigeria.

Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram hayatoi picha halisi ya maisha ya wananchi wa Nigeria, wanaojitahidi kuishi kwa amani na utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kiimani na kisiasa. Kinachonekana kwa sasa ni kinzani na misigano mikali kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini Nigeria. Haya ni matukio machache yanayochafua hali halisi ya maisha ya wananchi wa Nigeria.

Kumbe, kuna haja kwa watu kuangalia uhalisia wa maisha ya watu mjini na vijijini, wanavyoishi kwa kuheshimiana na kupendana kama ndugu. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali Barani Afrika kutokubali kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria wakati akichangia mada kwenye semina kuhusu uhuru wa kidini iliyokuwa imeandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani. Anasema, suluhu ya haki, amani na utulivu nchini Nigeria haiwezi kamwe kujikita katika mapambano ya mtutu wa bunduki, bali pia inapaswa kuangalia masuala ya kisiasa pamoja na majadiliano ya kidini, ili kweli haki na amani viweze kupatikana tena nchini Nigeria.

Si haba pia kwa Serikali pamoja na wadau mbali mbali ndani na nje ya Nigeria kuyaangalia mashambulizi haya katika jicho la umaskini na hali ngumu ya maisha, kwani vijana wasiokuwa na fursa za ajira ni kati ya makundi yanayotumiwa kuhujumu wananchi wa Nigeria. Inasikitisha kuona kwamba, hata baadhi ya vyama vya kisiasa nchini Nigeria vimekataa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali kuu ya Nigeria kwani vimewekeza kwenye Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram.

Kardinali Onaiyekan anasema, kwa sasa hata wanasiasa hawa wametambua kwamba, vita haina macho hata wao wameanza kuathirika kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria, kiasi kwamba, wameanza kuonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kushirikisha mchao wao. wamechelewa, lakini bado mchango wao unahitajika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa Mwaka 2014, watu zaidi ya elfu moja wameuwawa kikatili, wengine zaidi ya watu 446 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.