Jitahidini kuwa ni mashahidi amini wa Kristo na Kanisa lake!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 28 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na
Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar waliokuwa wanafanya hija yao ya kitume mjini
Vatican, hija inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Katika hotuba yake ambayo
amewakabidhi Maaskofu kutoka Madagascar, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Mama Kanisa
kuwa karibu zaidi na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana
hali na nafasi zao katika Jamii.
Amewewahimiza Maaskofu na waamini katika
ujumla wao, kuwa ni wajenzi na vyombo vya haki, amani na upatanisho nchini Madagascar
pamoja na kuhakikisha kwamba, wanawajengea uwezo maskini ili waweze kupambana na hali
yao ya maisha. Kanisa liwe mstari wa mbele anasema Baba Mtakatifu Francisko katika
kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia nchini Madagascar na kwamba,
maisha ya waamini yawe ni kielelezo cha wafuasi waamifu wa Kristo na Kanisa lake kwa
kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili.
Baba Mtakatifu anawaambia Maaskofu na
Mapadre kutoka Madagascar kwamba, wanapaswa kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani,
ili kweli maisha yao yaweze kuwa na mvuto na mashiko kwa watu wanaowahudumia, kwa
kuendelea kuwa ni wafuasi aminifu wa Kristo na Kanisa lake. Wawe daima mstari wa mbele
kutafuta: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na mafao ya wengi. Kwa namna
yoyote ile wasiwe ni sababu ya mgawanyiko wa kisiasa.
Baba Mtakatifu anawahimiza
Maaskofu wa Madagscar kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, kama sehemu ya mchakato
wa Uinjilishaji Mpya. Watoto wengi wenye umri wa kwenda shule, wapewe nafasi ya kusoma
na kuendelea na masomo yao. Wanafunzi walelewe na kukuzwa mintarafu maadili, utu wema
pamoja na tunu msingi za Kiinjili.
Wananchi wasaidiwe kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa wananchi wa Madagascar; walinde na kutetea
utu na heshima ya binadamu; wakuze utamaduni wa haki na amani, majadiliano na upatanisho
wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Madagascar kwa sasa na
kwa siku za usoni.
Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu wa Madagascar kwa kukazia
majiundo makini ya wanandoa watarajiwa. Anasema, Familia ya binadamu inakabiliwa na
vitisho pamoja na changamoto nyingi, kumbe haina budi kulindwa na kuendelezwa, ili
kutoa mchango wake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kwa kujenga watu wenye
ukomavu wanaoweza kuchangia katika tunu msingi za maisha ya kijamii, haki na amani.
Familia zisaidiwe katika hija ya maisha yake ya kiimani, ili ziweze kuwa kweli ni
shule ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti.
Baba Mtakatifu
anaendelea kuhimiza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo
na mafao ya wengi nchini Madagascar. Toba na wongofu wa ndani unaopata chimbuko lake
katika Maandiko Matakatifu ni changamoto endelevu ili kufikia maisha ya uzima wa milele.
Wakristo watolee ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Makleri na watawa
watambue kwamba, wao ni vyombo vya huduma kwa Mungu na Jamii. Kanisa liwe makini kuteuwa
vijana wanaoomba kujisadaka kwa ajili ya Upadre na Utawa. Wafundwe kuheshimu na kuthamini
mashauri ya Kiinjili; makini katika matumizi ya mali ya Kanisa kama kielelezo cha
Kanisa linalojali maskini na wanyonge.
Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna
ya pekee, Maaskofu kuwa karibu zaidi na Mapadre wao katika mahitaji yao ya kiroho
na kimwili. Anasema anawakumbuka wote katika maisha na utume wao, kwa kujisadaka kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake hata katika mazingira magumu. Pamoja na changamoto
zote za maisha, Mapadre wanapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wao, ili kuwatangazia
Injili ya Furaha. Maaskofu washirikiane na kushikamana na Mapadre wao ndani ya Kristo,
ili kwa pamoja, waweze kweli kusambaza harufu ya furaha inayobubujika kutoka katika
Injili ya Kristo.