Familia imepewa dhamana ya kutunza uhai na kuelimisha utunzaji bora wa mazingira!
Baraza la Kipapa la Familia kwa kushirikiana na Kikundi cha Greenaccord, Jumamosi,
tarehe 29 Machi 2014 limefanya semina maalum kuhusu mchango wa Familia katika utunzaji
wa mazingira, uliowashirikisha viongozi wa Makanisa, Serikali, Wachumi na Watetezi
wa mazingira. Imekuwa ni fursa pia ya kusikiliza ushuhuda uliotolewa na Familia moja
kutoka Napoli, kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na kuanza mchakato wa maisha
yanayoenzi utunzaji bora wa mazingira.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua
umuhimu na ushiriki wa Familia katika utunzaji bora wa mazingira ametuma ujumbe kwa
washiriki wa semina hii, kwa kusema kwamba, Familia kimsingi ni mahali maalum pa kutoa
hifadhi ya zawadi ya uhai na elimu makini kwa ajili ya kulinda na kutunza kazi ya
uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kwa ajili ya mafao ya sasa na kwa ajili ya kizazi
kijacho.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro
Parolin, katibu mkuu wa Vatican anayekazia umuhimu wa kutunza mazingira kwa ajili
ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawatakie washiriki wote wa semina hii heri na
baraka zake za kitume.