Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima
Niko nawe tena katika kipindi tafakari masomo Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima,
ambapo tunaalikwa kuwa watu wa mwanga. Katika somo la kwanza tunakutana na uteuzi
wa kiongozi atakayeongoza taifa la Israeli.
Mpendwa mwana
wa Mungu, jambo hili linatokea miaka 1000 kabla ya Kristu wakati ambao Waisraeli walikuwa
katika shida na taabu. Ili kuweza kuondokana na taabu hizi walilazimika kutafuta kiongozi
atakayewasaidia kuwaongoza ili waweze kupata ushindi toka Wafilistini. Kwa njia ya
Samueli Mungu anaonesha kijana mmoja toka Betlehem katika ukoo wa Yese, ambaye atapakwa
mafuta kwa ajili ya kuwa mfalme wao.
Basi Nabii atakwenda mpaka Betlehem na
kumwambia habari hii Yese ya kwamba mmojawapo wa wanawe amechaguliwa na Mungu kuongoza
taifa la Israeli. Yese anapokea habari hii kwa furaha kuu. Katika furaha hiyo, Yese
anafikiri na kuona kwa mtizamo wake, kuwa mtoto huyu atakuwa ELIABU. Katika hali ya
kawaida, Eliabu alikuwa mrefu na mzuri, tena alikuwa mtoto wa kwanza. Samweli anavutiwa
na sura ya Eliabu, lakini Mungu anasema hapana!
Kwa hapana ya Mungu, Yese
atalazimika kuwaleta watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa machungani! Mpendwa
msikilizaji, kati ya watoto hawa walioletwa hakukuwa na aliyechaguliwa na Mungu na
hivi Samueli akamwambia akamlete Daudi. Yese kwa kuamuliwa amlete Daudi alisema bado
Daudi ni mdogo kwa utume ambao ni mkubwa namna hii! Lakini Nabii atasisitiza kuwa
huyu ndiye chaguo la Mungu.
Mpendwa msikilizaji, katika uchaguzi huu tunagundua
kuwa njia za Mungu na njia zetu ni tofauti kabisa. Fikiria kwa kuchagua taifa la Israeli
liwe taifa teule aliacha taifa imara kiuchumi yaani Babilonia, akaacha Misri lililokuwa
taifa lenye ufundi wa hali juu na lenye watu wa dini, (Deut, 7:7-8). Ni katika mlengo
ule ule katika AJ Bwana atawachagua maskini, wadhambi, wanaoteswa, na wanaotengwa
kwa ajili ya ufalme wake. Kumbuka pia alipozaliwa watu wa kwanza kushuhudia utukufu
wake ni wachungaji waliokuwa kondeni. Mpendwa msikilizaji, ndiyo kusema hatuna mamlaka
ya kuingilia mpango wa Mungu, ni vema siku zote tukajisalimisha katika yeye kadiri
ya mapenzi yake.
Katika somo la Pili Mtakatifu Paulo anawaandikia Waefeso akisema,
kwa njia ya ubatizo wametwaliwa toka giza na kuingizwa katika mwanga. Kwa tendo la
kuingizwa katika utawala wa mwanga, wanaalikwa kuishi na kutenda matendo ya mwanga
na kuachana na matendo ya aibu. Anasonga mbele akisema lazima kukemea matendo yaliyo
ya aibu tena katika uwazi na kuyapatilizia mbali.
Katika Injili tunakutana
na picha ya kipofu anayeponywa na Bwana. Jambo la msingi na fundisho la Bwana ni kwamba
yeye amekuja kuwaondolea watu upofu wao na hasa upofu wa kiroho. Tunaona kabla ya
tendo hilo jema, wafuasi wake watamwuliza wakisema: Bwana, hivi ni nani kati ya mtoto
kipofu na wazazi wake aliyetenda dhambi mpaka mtoto yuko hivi?
Wanauliza swali
hili kwa sababu kulikuwa na imani kwamba Mungu huwaadhibu wenye dhambi na kuwarehemu
wema! Ndiyo kusema magonjwa na mikosi ilikuwa ni tokeo la dhambi! Aidha, aliyezalwa
katika shida kama hizo alidhihirisha kuwa dhambi ilitendwa na wazazi pamoja na mababu.
Mpendwa mwana wa Mungu, kufikiri hivi ni kinyume cha mapendo ya Mungu kwa watu, kwa
hakika Mungu hajui kuadhibu bali kupenda tu. Ndiyo kusema shida zilizopo zinakuja
kwa sababu ya uzembe wetu na hivi lazima tutafute suluhisho na namna ya kukabiliana
nazo.
Katika sehemu ya pili ya Injili tunaona sasa ukamilifu wa kile alichokifundisha,
yaani anakiweka katika matendo. Katia kutenda mwujiza wa kumfanya kipofu aone tena,
anatema mate chini na kufanya tope ambalo atampaka kipofu. Baada ya hilo anamwambia
nenda kanawe katika birika ya Siloamu na kwa kufanya hivyo kipofu anaona! Mpendwa
msikilizaji, kuna nini katika matendo haya? Mambo yako hivi kwa sababu watu wa wakati
huo waliamini katika pumzi kuwako na roho na katika mate kulijaa nguvu ya mtu.
Ndiyo
kusema Bwana anatumia alama zilezile kutenda kazi yake ya kuleta uhuru kwa kipofu.
Bwana haishii tu katika alama hizi za mwanzo bali anamwambia nenda ukanawe katika
Siloamu, ndiyo kusema anamtuma. Hapa tunaona Bwana aliyetumwa na Mungu anamwalika
mtu kuja kwake ili apate maji ya uzima, maji yanayoponyesha kama alivyomwahidia mwanamke
msamaria, na kisha kwenda kutangaza habari njema ya furaha.
Baada ya tendo
hili la uponyaji kipofu ataulizwa na watu mbalimbali kuhakikisha ni kwa nguvu ya nani
amepona. Wa kwanza ni majirani zake ambao wanajiuliza ni yeye au ni mwingine na baadaye
watampeleka kwa Mafarisayo ambao watamlalamikia Bwana badala ya kumsifu, ati kwa sababu
alitenda kazi hiyo wakati wa Sabato, na kwa jinsi hiyo Bwana hakutoka kwa Mungu. Katika
hili wengine walisema lakini inawezekanaje mwenye dhambi afanye mwujiza huu?
Kwa
majirani kipofu atasema mimi ndiye na wala si mwingine. Kwa Mafarisayo atasema yakuwa
aliyeniponya ni Nabii. Mpendwa msikilizaji, katika kuendelea kutafuta ukweli, wenye
madaraka watawaendea wazazi wake na kuwauliza na wazazi kwa woga wa kutengwa watasema
kamwulizeni yeye mwenyewe kwa kuwa ni mtu mzima. Wenye mamlaka watamrudia aliyekuwa
kipofu wakitaka akane ukweli na yeye atawaambia ninachojua ni kwamba nilikuwa kipofu
na sasa ninaona. Ndugu huyu aliendelea kutetea ukweli huo kwa furaha mpaka mwisho.
Mpendwa, katika hili twajifunza kuwa wakweli na kuwa wenye furaha daima, na
hivi kusimamia imani na matendo makuu ya Mungu. Ndiyo kusema furaha na neema za Mungu
tulizozipokea kwa njia ya ubatizo na kipaimara twapaswa kuzitunza mpaka mwisho wa
nyakati. Tena, katika safari ya kulinda imani kutakuwa na wakati wa furaha na mateso,
jambo kuu ni kuweka tumaini katika yeye aliyetuponya.
Mpendwa ninakutakia
furaha na matumaini katika maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa nguvu zake
kukua na kusimamia imani uliyoipokea kama zawadi toka kwake.
Tumsifu Yesu
Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.