2014-03-28 15:26:17

Rais Karolos Papoulias akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 28 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Karolos Papoulias kutoka Jamhuri ya watu wa Ugiriki, ambaye pia alibahatika kukutana kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wameridhika na uhusiano uliopo kati ya Vatican na Nchi ya Ugiriki, unaojikita katika kutafuta mafao ya wengi, uhuru wa kuabudu pamoja na kudumisha mchango wa dini katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ugiriki. Wameridhika na mchango unaofanywa na dini mbali mbali nchini humo pamoja na Makanisa kuendeleza majadiliano ya kiekumene.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamejikita zaidi katika kupembua athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na mchango wa nchi ya Ugiriki kwenye Umoja wa Nchi za Ulaya. Mwishoni, viongozi hawa wawili wameonesha wasi wasi wao juu ya hatima ya Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea kujitokeza katika ukanda huu, bila kusahau kinzani zilizopo sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.