Utakatifu ni changamoto na mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa ajili ya watu wachache
waliobahatika katika hija ya maisha yao. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi
Mungu ni Mtakatifu, kumbe hata waamini wanapaswa kuchuchumilia utakatifu wa maisha,
kila mtu kadiri ya wito, maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Waamini wanapaswa kumfuasa
Yesu Kristo ambaye alikuwa ni fukara, mnyenyekevu aliyethubutu kuubeba Msalaba, ili
kuwashirikisha waamini katika utukufu wake.
Hivi ndivyo
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanavyoandika katika Hati ya Mtaguso mkuu
kuhusu Kanisa, Lumen Gentium, yaani Mwanga wa Mataifa. Huu ni mwelekeo mpya uliobainishwa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI
katika Katekesi yake ya tarehe 13 Aprili 2011 anawaalika waamini kuitafuta na kuanza
hija inayoelekea katika utakatifu wa maisha kwa kutambua kwamba, maisha matakatifu
si juhudi na nguvu za mtu binafsi, bali ni baraka na neema inayotolewa na Mwenyezi
Mungu ambaye ni Mtakatifu wa watakatifu anayewawezesha waamini kuwa ni watakatifu.
Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayemwalika mwamini kutoka katika undani wa maisha
yake kwa kumkirimia neema inayomletea toba na wongofu wa ndani.
Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican unakumbusha kwamba, Wafuasi wa Kristo wanaitwa kumfuasa Kristo
kwa vile wameitwa na Mwenyezi Mungu kadiri ya mpango na neema inayowahesabia kuwa
haki mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya imani katika Ubatizo, Wakristo wanafanyika
kuwa ni Watoto wa Mungu wanaoshirikishwa utukufu, ukuu na umungu wa Kristo. Wakristo
wanashiriki katika Fumbo la Pasaka kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Roho
Mtakatifu.
Kwa njia ya Ubatizo anasema Mtakatifu Paulo, mwamini ameifia dhambi,
akazikwa na kufufuka pamoja na Kristo, kiasi kwamba, maisha ya Mkristo yanapaswa kufungamana
na Kristo, tayari kuanza hija inayomwezesha mwamini kutembea katika mwanga wa Kristo
Mfufuka. Lakini anakumbusha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Mwenyezi Mungu anapenda
kuheshimu uhuru wa kila binadamu. Anamtaka mwamini mwenyewe kukubali na kushiriki
katika mpango wake kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ambao mwamini anakirimiwa
kama zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Utashi wa binadamu hauna budi kuenda sanjari
na utashi wa Mungu, ili hatimaye, kufikia utakatifu.