2014-03-28 14:58:05

Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 28 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na washiriki wa kozi maalum iliyokuwa imeandaliwa na Baraza la Toba ya Kitume, iliyowashirikisha Mapadre wapya na Mashemasi kama sehemu ya majiundo makini kwa waungamishaji wa baadaye, kwa kutambua thamani ya utume huu ambao wanakabidhiwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaalika washiriki wa kozi hii kuhakikisha kwamba, wanatumia uzoefu, mangamuzi na ugunduzi makini ili kulisaidia Kanisa na waungamishaji kutekeleza utume wa huruma ya Mungu ambao ni muhimu sana. Wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho watambue kwamba, mhusika mkuu katika Sakramenti ya Upatanisho ni Roho Mtakatifu anayemkirimia mwamini maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Waungamishaji wanachangamotishwa kuwa ni watu wa Roho Mtakatifu, mashahidi na watangazaji makini na wenye furaha juu ya ufufuko wa Kristo, mambo yanayojidhihirisha katika Sakramenti ya Upatanisho.

Padre muungamishaji awapokee waamini kwa upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Wao ni Mahakimu na Waganga wa mioyo ya waamini, kwa kuponya na kuwaondolea watu dhambi zao.

Baba Mtakatifu anasema, Sakramenti ya Upatanisho inamkirimia mwamini maisha mapya pamoja na kuboresha neema ya Sakramenti ya Ubatizo, mwaliko wa kuwapatia waamini neema hii kwa moyo mkuu. Mapadre wawahudumie waamini wao kwa kuhakikisha kwamba, wanatenga muda wa kutosha sanjari na kuwa na maisha bora ya kiroho, kwani huruma ni kiini cha Injili.

Ni mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayempenda mdhambi na kumwalika kutubu na kuongoka. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, waamini wanapata shida katika kukimbilia kiti cha maungamo ili kuungama dhambi zao kwa binadamu mwenzao. Kutokana na ukweli huu, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Mapadre hawawi vikwazo kwa waamini katika kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Mapadre wawe na busara katika kutoa Sakramenti ya Upatanisho, wawe wasikivu na kuwasaidia waamini kuweza kujipatanisha na Mungu. Kiti cha maungamo iwe ni fursa ya kuonja msamaha na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, Sakramenti ya Upatanisho ni zawadi ya Kristo kwa Kanisa lake, ili kuwawezesha waamini kupokea huruma ya Mungu.

Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inaadhimishwa kikamilifu, kwani ni chemchemi ya huruma na wokovu. Mapadre wajipange barabara ili kutoa nafasi kwa waamini kuungama dhambi zao, wakitambua kwamba, uaminifu unazaa matunda mwengi. Nyumba za kitawa zijitahidi kuwa na Mapadre ambao wanaweza kuungamisha watu kwa muda mrefu zaidi. Baba Mtakatifu anawatakia Mapadre wote neema na baraka ya kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.