Rais Obama akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko siku ya Alhamisi tarehe 27 Machi 2014 majira ya asubuhi,
amekutana na kuzungumza na Rais Barack Obama wa Marekani pamoja na ujumbe wake. Baadaye,
Rais Obama alikutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua
ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje
na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Katika mazungumzo ya viongozi hawa
wawili, wamebadilishana mawazo kuhusu masuala tete yanayoendelea kujitokeza katika
Jumuiya ya Kimataifa na kwamba; maeneo yanayokabiliana na vita pamoja na kinzani za
kijamii yanapaswa kuheshimu haki msingi za binadamu sanjari na haki za kimataifa;
majadiliano yapewe kipaumbele cha pekee katika kufikia suluhu ya kinzani hizi.
Rais
Obama pamoja na Baba Mtakatifu wamegusia pia ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali
pamoja na kukiri kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mafao ya
wengi na kwamba, uhuru wa kidini, maisha, uhuru wa kidhamiri na mabadiliko katika
sheria za uhamiaji ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji
wake.
Kwa pamoja, viongozi hawa wamekubaliana kimsingi kwamba, kuna haja ya
kusimama kidete kupambana kufa na kupona dhidi ya biashara haramu ya binadamu ulimwenguni.