2014-03-27 12:07:47

Changamoto katika maisha na utume wa Kanisa nchini Madagascar


Maaskofu Katoliki kutoka Madagascar, kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 29 Machi 2014 wako kwenye hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Varican. Kanisa Katoliki Madagascar lina Majimbo makuu matano yanayoundwa na Majimbo kumi na saba. Maaskofu hawa, Alhamisi, tarehe 27 Machi 2014 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Madascar ni nchi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imejikuta ikitumbukia katika machafuko ya kisiasa na kinzani za kijamii. Kwa sasa lengo ni kuona kwamba, wananchi wote wa Madagascar wanajikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho. Maaskofu wanapenda kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema misingi ya haki na amani pamoja na kujikita katika kutafuta mafao ya wengi.

Kama sehemu ya mchakato wa waamini kuhakikisha kwamba, wanayafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa tayari kujikita katika harakati za kuyatakatifuza malimwengu, Maaskofu wamefanya tafsiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa katika lugha ya Kimalagashi. Kanisa lina matumaini makubwa kwa waamini wake, licha ya changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza nchini humo. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya vyombo vya habari, kama njia ya kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhabarisha Jamii.

Mwaka 2015, Kanisa nchini Madagscar litaadhimisha Mwaka wa Vijana, ili kuwajengea uwezo wa kushuhudia Injili miongoni mwa vijana wenzao. Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika mjini Vatican ni fursa nyingine ya kuangalia fursa, changamoto na matatizo yanayozikabili nchini Madagascar. Maaskofu wanasema, nchini humo wanakabiliana na wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, jambo ambalo linawanyima matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baadhi ya watoto hawa wametumbukizwa katika biashara ya ngono, hali inayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu.

Kanisa Katoliki Madagascar linaendelea kujielekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upatanisho na mafao ya wengi. Wingi wa madhehebu ya Kikristo nchini humo ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki. Hapa Maaskofu wanasema, kuna haja ya kukazia majiundo makini ya Katekisimu, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Biblia, ili vijana waweze kuwa na msingi thabiti wa imani yao ya Kikristo bila kuyumbishwa yumbishwa.

Umaskini, ukosefu wa fursa za ajira na magonjwa ya muda mrefu ni kati ya mambo yanayowasukuma Wakatoliki kukimbilia kwenye Madhehebu mbali mbali ya Kikristo wakiwa na tumaini kwamba, wanaweza kupata muujiza utakaokata mzizi wa fitina katika maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.