2014-03-26 08:03:46

Rais Obama atinga mjini Roma tayari kukutana na Papa Francisko!


Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Serikali ya Marekani unapania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha misingi ya haki, Amani na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa. Nchi hizi mbili mwaka 2014 zinaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu zilipoanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia. RealAudioMP3
Lakini itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1788 Rais George Washington wa Marekani alimwambia Papa Pio wa Sita kwamba, kulikuwa hakuna umuhimu wa Serikali ya Marekani kuridhia uteuzi wa Maaskofu kwani uhuru wa wananchi wa Marekani ulipania kuwakomboa wananchi wake na kuimarisha uhuru wa kidini.
Baba Mtakatifu Pio wa sita, akamteua Padre John Carroll, Myesuit kuwa ni Askofu wa kwanza nchini Marekani. Huu ukawa ni mwanzo wa uwepo wa Hirakia ya Kanisa nchini Marekani na Jimbo la kwanza likawa ni Baltimore, leo hii Marekani ina majimbo 200 yanayounda Kanisa Katoliki. Kilipita kitita cha miaka kabla ya Marekani na Vatican kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia! Ilikuwa ni Mwaka 1984 Rais Ronald Reagan na Mwenyeheri Yohane Paulo II wakaanzisha uhusiano wa Kidiplomasia ambao unaendelea kuimarika siku hadi siku.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 30 tangu Serikali ya Marekani na Vatican walipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Kunako mwaka 1965 Papa Paulo VI alitembelea kwa mara ya kwanza New York. Mwenyeheri Yohane Paulo II katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro akatembelea Marekani mara saba na kunako Mwaka 2008, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea Marekani pamoja na kuhutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa mara ya kwanza Rais Woodrow Wilson, Rais wa Marekani alitembelea Vatican kunako mwaka 1919, tangu wakati huo, Marais mbali mbali wa Marekani wametembelea na kukutana na Mapapa mjini Vatican. Rais Barack Obama alimtembelea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2009 na kwa sasa anatarajiwa tena kukutana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ziara yake ya kikazi Barani Ulaya, mwishoni mwa Mwezi Machi, 2014.
Serikali ya Marekani na Vatican zimeendelea kujenga na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa kutambua kwamba, Marekani ni kati ya wadau wakuu katika masuala ya kimataifa na Vatican kimsingi imekuwa ni sauti ya kinabii kwa watu na mataifa yasiokuwa na sauti. Kanisa limeshirikishana na Jumuiya ya Kimataifa: furaha, matumaini na majanga mbali mbali katika maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika na kuwahimiza viongozi wa Kanisa na waamini kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, ili kuweza kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda amini pamoja na kuendelea kuwamegea watu Injili ya Furaha.
Baba Mtakatifu anaendelea kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa ili kubadilishana uzoefu na mang’amuzi yanayopania kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu, haki na amani kati ya watu wa mataifa. Vatican itaendeleza mchakato wa majadiliano ya kina na ukweli pamoja na Serikali ya Marekani katika masuala mbali mbali ya kimataifa na kitaifa.
Askofu mkuu Dominique Mamberti anasema kwamba, Kanisa linapenda kushiriki katika mchakato wa majadiliano, ili kulinda na kutetea zawadi ya uhai, utu na heshima ya binadamu; haki, amani, uhuru wa kidini na maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linapania kujikita katika harakati za kutafuta mafao ya wengi.
Ni matumaini ya Vatican kwamba, uhusiano wa kidiplomasia ambao umekuwepo hata kabla ya mwaka 1984, utaendelea kudumisha urafiki na majadiliano katika Familia ya Kimataifa, ili kweli dunia iweze kujengeka kwa kuimarisha misingi ya haki, amani na udugu.

Taarifa hii imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.