2014-03-26 07:43:10

Njia ya Msalaba, 2014: mwaliko wa kuiangalia sura ya Kristo katika sura ya mwanadamu anayeteseka!


Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa kuu kwa Mwaka 2014 imeandaliwa na Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso Boiano, Italia. Ni tafakari ambayo ameifanya kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na itafanya rejea kwa vituo kumi na vinne vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo.

Askofu mkuu Bregantini ni mwenyekiti wa Tume ya masuala ya kijamii, kazi, haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Taarifa hii imetolewa muda mfupi tu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kusali pamoja na wahanga wa mashambulizi ya kikundi cha kigaidi cha Mafia nchini Italia.

Katika mikakati yake ya kichungaji, Askofu mkuu Bregantini amekuwa akijielekeza zaidi katika majiundo ya dhamiri nyofu, kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu; haki msingi, amani na utawala wa sheria.

Askofu mkuu Bregantini anasema, amepewa heshima kubwa na Baba Mtakatifu Francisko kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kwa mwaka 2014. Ni tafakari inayoonesha Fumbo la Msalaba katika maisha ya Yesu mintarafu mahangaiko na mateso ya mwanadamu, katika sala na tafakari.

Hapa waamini wanaalikwa kuingalia sura ya Kristo katika sura ya mwanadamu anayeteseka. Yesu anaendelea kumwonjesha mwanadamu huruma na upendo wake wa dhati; anayafuta machozi ya watu wake kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro alipomkana mara tatu. Tafakari ya Njia ya Msalaba pamoja na mambo mengine itagusia athari za myumbo wa uchumi kimataifa, umuhimu wa Neno la Mungu.

Ikumbukwe kwamba, Askofu mkuu Bregantini ni mwanashirika wa Shirika la Madonda Matakatifu, maarufu kama Wasigmatin. Ni mwaliko wa kumwilisha Injili ya Furaha katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu anayejikuta daima akisukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mama Kanisa anapenda kumwonjesha mwanadamu upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani inayobubujika kutoka kwa Yesu na Kanisa lake!







All the contents on this site are copyrighted ©.