2014-03-26 07:27:34

Inapendeza kwa Waislam na Wakristo kusali pamoja kwa Bikira Maria!


Baba Mtakatifu Francisko anatawatakia kheri na baraka wanafunzi wote waliosoma katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yosefu na Chuo cha Jamhour, wakati huu wanapoadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, inafurahisha kuona kwamba, Wakristo na Waislam wanaungana kwa pamoja kwa ajili ya kutoa heshima kwa Bikira Maria. Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Lebanon yaliyoko Harissa ni mahali ambapo, waamini wa dini mbali mbali wanaweza kukusanayika kwa ajili ya kusali na kumwomba Bikira Maria.

Huu ni jumbe ambao umeandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na kusomwa na kusomwa na Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, katika Ibada ya pamoja kati ya Waislam na Wakristo, huko Lebanon, Jumanne, tarehe 25 Machi 2014.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka wananchi wote wa Lebanon chini ya usimamizi na ulinzi wa Bikira Maria Mama Yetu wa Lebanon, ili waendelee kutunza urithi walioupokea kwa kujikita katika majadiliano na wote; kwa kuheshimiana pamoja na kudumisha umoja na udugu kati ya watu.

Baba Mtakatifu anawahimiza Wakristo na Waislam kufanya kazi kwa pamoja ili kujenga na kudumisha amani, mafao ya wengi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na ujenzi wa Jamii nzima. Baba Mtakatifu anawaweka wananchi wote chini ya ulinzi na tunza ya kimama ya Bikira Maria, Malkia wa Amani.









All the contents on this site are copyrighted ©.