2014-03-26 08:55:11

Familia ni mhimili mkuu wa maendeleo endelevu ya binadamu!


Huduma makini kwa familia inayojikita katika: akili, ujasiri na upendo wa dhati, ndiyo mambo msingi yanayobainishwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia wakati wa kuzindua maandalizi rasmi ya Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015.

Mama Kanisa anapenda kuweka mikaka makini inayojikita katika ujasiri ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Upendo wa dhati unapania kuvuka vikwazo vilivyopo katika maisha ya ndoa na familia kwa kuzingatia Injili ya Familia na Maisha ya mwanadamu.

Uzinduzi wa Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya nane ya Familia Kimataifa yamehudhuriwa pia na Askofu mkuu Charles Joseph Chaput, kutoka Jimbo kuu la Philadelphia Marekani pamoja na ujumbe wake, watakaokuwa ni wenyeji wa maadhimisho hayo. Hii ni fursa makini kwa Mama Kanisa kuweza kujikita zaidi katika taalimungu ya maisha ya ndoa na familia; tasaufi na utakatifu wa maisha kati ya wanandoa; Kanisa na Familia; Familia na Tamaduni mamboleo pamoja na changamoto zake; Familia na tatizo la uhamiaji; Familia na Majadiliano ya kidini na kiekumene.

Hizi ni kati ya changamoto msingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa Familia, kwa kujikita katika mikakati thabiti na yenye akili, ujasiri na upendo mkamilifu kwa maisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa analionesha hili kwa kuitisha Sinodi maalum na ile ya kawaida kwa ajili ya Familia, kwa kutambua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa, kama ilivyojionesha katika kikao cha Baraza la Makardinali kilichohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa huko Philadelphia, Marekani ni sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia. Familia ni tema inayojadiliwa pia kwenye Umoja wa Mataifa, kwani Mwaka 2014, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Mwaka wa Familia. Kumbe hili ni tukio ambalo linalishirikisha Kanisa Katoliki nchini Marekani, lakini pia lina mwelekeo mpana zaidi kwani uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, utakoleza mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kifamilia.

Huu ni mwaliko anasema, Askofu mkuu Paglia kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa pamoja ili kuweza kuipatia Familia kipaumbele cha pekee, ili kujenga na kuimarisha udugu, upendo na mshikamano wa dhati kati ya binadamu, ili kweli familia ya binadamu iweze kujisikia kuwa ni wamoja.

Askofu mkuu Chaput amewasili mjini Vatican akiwa na ujumbe mzito wa wadau kutoka katika vyama vya kitume vinavyojihusisha na maisha ya kifamilia pamoja na wanasiasa ambao kwa pamoja wanalenga kufanikisha maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa. Anasema, maadhimisho haya ni fursa ya neema na furaha kwa Kanisa zima kwa kutambua kwamba, familia ni kikolezo makini cha maendeleo endelevu ya mwanadamu.

Kanisa na Jamii kwa ujumla hawana budi kushirikiana kwa ajili ya kuboresha maisha ya familia, kwa kutunga sera makini pamoja na kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayozikabili familia nyingi duniani. Jimbo kuu la Philadelphia linaendelea kuboresha miundo mbinu na mahudhui yatakayofanyiwa kazi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa.

Katika uzinduzi wa maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, baadhi ya waamini na wakereketwa wa maisha ya ndoa na familia kutoka Marekani, wametoa ushuhuda wao, kuhusu umuhimu wa maisha ya ndoa na familia ndani na nje ya Kanisa, kwani familia ni shule ya utakatifu, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Tunu msingi za maisha ya kifamilia zikiboreshwa, dunia inaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.







All the contents on this site are copyrighted ©.