Endeleeni kusali ili Jumuiya za Waamini zisitindikiwe na Mapadre wema, watakatifu
na wachapakazi
Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ambazo zinamwingiza
mtu katika Ukristo na kuwashirikisha watu hali ya kimungu kwa njia ya Yesu Kristo
na hivyo kuwafungulia mlango wa wokovu. Huu ndio wito wa kwanza kabisa unaowashikamanisha
wafuasi wote wa Kristo ndani ya Kanisa. Sakramenti ya Daraja Takatifu na Ndoa Takatifu
ni Sakramenti za ushirika na kwa ajili ya wokovu wa watu wengine na zinachangia pia
wokovu wa mtu binafsi kwa njia ya huduma kwa wengine na ujenzi wa Kanisa la Kristo
Ni utangulizi uliofanywa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake,
Jumatano, tarehe 26 Machi 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini
Vatican pamoja na kuendelea kupembua Sakramenti ya Daraja Takatifu. Papa anasema,
Daraja takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa mitume
wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati: hivyo hii ni Sakramenti
ya huduma ya kitume nayo ina ngazi kuu tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema wale walioteuliwa na kuwekwa wakfu wanaendeleza huduma
ya Roho wa Kristo ndani ya nyakati na kuonesha uwepo wa Kristo ambaye ni Mwalimu na
Mchungaji mwema. Makleri waliwekwa wakfu ni wakuu wa Jumuiya ya Kikristo wanaopaswa
kutambua kwamba, wao ni wahudumu, kama Yesu mwenyewe alivyoonesha katika maisha na
mafundisho yake, kwani Yeye alikuja si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia na kuyatoa
maisha yake ili yawe ni fidia kwa wengi.
Padre anapaswa kuwa na upendo mkubwa
kwa Kristo na Kanisa lake, kama vile ambavyo Kristo alilipenda Kanisa lake kiasi cha
kujisadaka na kulitakatifuza, kwa njia ya Maji na Neno, ili kuonesha utukufu wa Kanisa
pasi na mawaa. Padre anapaswa kujisadaka kwa akili na moyo wake wote bila hata ya
kujibakiza. Hii ndiyo familia yake ambayo kamwe hapaswi kuibinafisha. Baba Mtakatifu
anasema, Yesu Kristo ndiye mchumba pekee na mwaminifu wa Kanisa lake na yote ni mali
yake!
Baba Mtakatifu anasema, maisha ya Kipadre ni mwaliko wa Padre kumwilisha
ile zawadi iliyoko ndani mwake, aliyoipokea kwa njia ya Neno na kuwekewa mikono. Maisha
ya Kipadre hayana budi kurutubishwa kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Adhimisho
la Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na kupokea mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho,
ili kujenga na kuimarisha upendo na mshikamano pamoja na Yesu, vinginevyo, Padre anaweza
kujikuta akimezwa na malimwengu.
Padre atambue kwamba, daima anahimizwa kumwongokea
Mwenyezi Mungu na kukimbilia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake; hapa ni
mahali pa kuchota nguvu na mfano unaopaswa kutolewa kwa ndugu zake katika Jumuiya.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili
ya kuwaombea wale wote wenye Daraja Takatifu katika Kanisa, lakini zaidi wale wanaokabiliana
na hali ngumu ya maisha; watu ambao wako katika mchakato wa kutafuta tena upya wa
maisha ya wito wao.
Baba Mtakatifu anawaomba waamini kuendelea kusali ili
kamwe, Jumuiya za waamini zisitindikiwe na wachungaji wema na watakatifu, mintarafu
Moyo wake mtakatifu. Wawe ni viongozi kadiri ya Maandiko Matakatifu, waaminifu kwa
Kristo na Kanisa lake; makini katika huduma kwa binadamu, daima wakijitahidi kufuata
mfano wa Kristo Mchungaji mwema, aliyethubutu kuwaosha miguu Mitume wake na hatimaye,
akajimimina pale juu Msalabani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu wakati akizungumza na mahuaji pamoja na wageni kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, ameendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea
kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na mshikamano wa kidugu kati
ya watu. Bikira Maria Mama wa Mungu ambaye, Kanisa limemsherehekea kwa kupashwa habari
kuwa Mama wa Mungu, awasaidie vijana kuwa wasikivu wa utashi wa Mungu katika maisha
yao kama alivyofanya Bikira Maria.
Wagonjwa wasikatishwe tamaa na magumu wanayokabiliana
nayo katika hija yao ya maisha, kwani Mwenyezi Mungu hawezi kuwapatia Msalaba mkubwa
unaozidi nguvu na uwezo wao. Wanandoa wapya wajenge maisha yao katika msingi wa Neno
la Mungu.