2014-03-25 12:22:55

Wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopokelewa kwa moyo mnyofu kama alivyofanya Bikira Maria


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba atakuwa ni Mama wa Mungu, Ibada iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku ya Jumanne, tarehe 25 Machi 2014 anasema kwamba, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopokelewa kwa moyo wa unyenyekevu kama alivyofanya Bikira Maria.

Ni changamoto kwa waamini kusimama kidete kupambana kufa na kupona na Shetani, ili kuepuka nafasi za dhambi na vishawi, vilivyopelekea Adam na Eva kuanguka katika dhambi ya asili kwa kukosa utii kwa Mwenyezi Mungu. Tangu wakati huo, Mwenyezi Mungu akaamua kufanya hija na binadamu kwa njia ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Waamini wanahimizwa kuwa wasikivu na wanyenyekevu kwa Neno la Mungu ambalo ni dira na taa katika mapito yao.

Bikira Maria alionesha moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kwa mpango wa Mungu katika maisha yake, hiki ndicho kiini cha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu; Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, na kukaa kati ya watu wake, ili kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Siku kuu ya leo ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa kuwakirimia binadamu ukombozi.







All the contents on this site are copyrighted ©.