2014-03-25 10:25:24

Watangazieni watu Injili ya Familia na Uzuri wake!


Ndoa na familia ni mada iliyokuwa inapembuliwa kwa kina na mapana na wanafunzi pamoja na majaalimu wao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, katika semina iliyoandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, (CCEE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II hapa mjini Roma. Wajumbe wameangalia kwa umakini mkubwa urithi ambao Mwenyeheri Yohane Paulo II ameliachia Kanisa katika mafundisho yake kuhusu Ndoa na Familia.

Wajumbe wanasema kwamba, kuna utajiri mkubwa wa Mafundisho ya Mwenyeheri Yohane Paulo II, kama yakitumika barabara yanaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto katika maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Semina hii imeratibiwa na Kardinali Lorenzo Baldiseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu Katoliki.

Wajumbe wanasikitika kusema kwamba, kuna umati mkubwa wa waamini ambao hawafahamu kwa undani Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia. Haya yamejidhihirisha hata katika majibu ya maswali dododo kuhusu ndoa na familia kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2014. Wanasema, dhamana na utume wa Kanisa kwanza kabisa na kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwapatia watu fursa ya kukutana na Yesu, ili kuwakirimia utimilifu wa maisha. Ni Kristo anayeokoa Familia kwa njia ya Kanisa lake.

Wajumbe na wahamasishaji wakati wa Semina hii kwa pamoja wameangalia changamoto katika maisha ya ndoa na familia na kukiri kwamba, umefika wakati kwa Mama Kanisa kuwaonjesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwa kuwatangazia Injili ya Familia, kwa kujikita katika ukweli unaofumbatwa ndani ya moyo wa mwanadamu.

Kardinali Baldisserri amewashauri wajumbe wa Semina hii kutumia kipindi hiki cha maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia, kuzungumzia kuhusu umuhimu wa Familia katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuwashirikisha wengine Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia, yanayopaswa kutolewa ushuhuda katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Sinodi ijayo, itajikita zaidi katika Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia, kama njia ya kukukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa sasa. Familia za Kikristo zihamasishwe kuwapeleka watu kwa Kristo na Kanisa lake.

Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, linatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Yohane Paulo II kwa ajili ya kulinda, kutetea na kuendeleza Familia. Waraka wa Kitume, Wajibu wa Familia za Kikristo, Familiaris Consortio, bado ni Waraka muhimu sana katika kukabiliana na changamoti za maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Waraka huu ni Katekesi juu ya upendo wa kibinadamu, wanakiri wajumbe wa Semina hii.

Mwenyeheri Yohane Paulo II ameutangazia ulimwengu ujumbe makini wa Ndoa na Familia inayopaswa kusherehekewa katika mwanga wa neema ya Mungu, kwa kuendelea kutangaza Injili ya Familia na uzuri wake, hata kama itapingana na mawazo ya watu wa nyakati hizi.

Kanisa liwasindikize wanafamilia ili waweze kuwatangazia jirani zao ukweli na upendo wa maisha ya ndoa na familia unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Familia ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa mahalia. Hii ni changamoto kwa Wakristo kujitosa kimasomaso kutangaza Injili ya Furaha kama ambavyo anaendelea kuhimiza Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati hizi.

Washiriki wa semina hii, walikwenda kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kutoa heshima yao kwa Mwenyeheri Yohane Paulo II kwa njia ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Carlo Caffarra, Rais wa kwanza wa Taasisi ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II, kuzunguka kaburi la Mwenyeheri Yohane Paulo II, lililoko ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.