Wananchi wanaelemewa na umaskini, wanahitaji kuona ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
watu!
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, ni muda muafaka wa kumtafuta Mungu
ili kuweza kujipatanisha naye pamoja na jirani. Ni wakati wa kuimarisha ari na moyo
wa kimissionari, ili kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Myumbo wa uchumi
kimataifa unaendelea kusababisha umaskini mkubwa wa hali na kipato, kiasi kwamba,
kuna maelfu ya watu hawana uhakika wa kupata mahitaji yao msingi kutokana na ukosefu
wa fursa za ajira.
Ni changamoto kwa Serikali ya Italia kuhakikisha kwamba,
inajielekeza zaidi katika uzalishaji na upatikanaji wa fursa za ajira ili kuwajengea
vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora, kwani kwa sasa wengi wao wamekata tamaa!
Mkakati huu unawezekana ikiwa kama, Serikali itaendelea kubana matumizi kwa kuwekeza
zaidi katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.
Hayo yamesemwa na Kardinali
Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wakati wa kufungua mkutano
mkuu wa Kamati kuu la Baraza la Maaskofu Italia, siku ya Jumatatu, tarehe 24 Machi
2014. Anasema, athari za myumbo wa uchumi kimataifa umepelekea pia mpasuko wa maisha
katika familia nyingi nchini Italia na kwamba, hali ya umaskini wa hali na kipato
inazidi kuongezeka kwa kasi kubwa nchini Italia. Huu ni umaskini unaojikita katika
maisha ya kiroho na adili.
Baraza la Maaskofu Katoliki linalaani vitendo vya
uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa wenye misimamo mikali, inayojikita
katika ubinafsi, bila kuzingatia utu na heshima ya binadamu; usawa na haki. Kila mtu
anayo haki ya kujieleza, lakini pia anapaswa kuwaheshimu wengine. Kuna haja kwa wanasiasa
nchini Italia kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa
mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.
Watu waondokane na ubinafsi usiokuwa na mashiko kwa kujenga na kuimarisha udugu, umoja
na mshikamano.
Kardinali Bagnasco anasema kuna haja ya kuelimisha akili na
moyo, kwa kukazia dhamiri nyofu na uhuru wa kuabudu. Wazazi na walezi wana haki ya
kuchagua elimu wanayotaka kwa ajili ya watoto wao, ndiyo maana, hapo tarehe 10 Mei
2014, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Wazazi, Walezi, wanafunzi pamoja na watu
wenye mapenzi mema, wataungana na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro kukazia umuhimu wa: maisha, familia na elimu makini kwa watoto.
Kardinali Bagnasco anawaalika wazazi na walezi kusimama kidete kulinda na kutetea
haki zao msingi.