Vitendo vya kigaidi nchini Kenya vinaendekezwa na umaskini miongoni mwa vijana!
Askofu Emmanuel Barbara wa Jimbo Katoliki Malindi na Msimamizi wa kitume Jimbo kuu
la Mombasa, Kenya anasema, mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza kwenye
mwambao wa Pwani ya Mombasa yanatishia amani na usalama kwa wananchi wote wa Kenya
na wala si tu kwa Wakristo.
Jumapili iliyopita, watu sita walifariki dunia
na wengine ishirini na moja kujeruhiwa vibaya baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni
kikundi cha Kigaidi kuvamia na kulipua Kanisa la Kiinjili huko Likoni. Inasadikiwa
kwamba, vikundi hivi vya kigaidi vinafadhiliwa na baadhi ya wafanyabiashara wa Mombasa
kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Kuna vijana kutoka Somalia na Kenya wanaopewa
fedha ili kufanya vurugu na wala si kwamba, ni waamini wenye msimamo mkali wa kidini
kama wanavyotaka kuwasadikisha wananchi wengi wa Kenya. Askofu Barbara anasema, kuna
haja kwa watu kutubu na kuongoka ili kuachana na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea
kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.