2014-03-25 07:53:35

Ushuhuda wa mshikamano wa upendo na udugu ni kikolezo cha Uinjilishaji Mpya


Utengano kati ya Wakristo, umaskini na hali ngumu ya maisha; vita na kinzani za kikabila, kisiasa na kidini ni kati ya mambo yanayokwamisha mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Kuna haja kwa Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kweli za Kiinjili zinapaswa kutangazwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo unaodhihirishwa na Wakristo wote.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu kutoka Guinea Conakry, Afrika Magharibi ambao kwa sasa wanaendelea na hija yao ya kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, umoja na mshikamano hauna budi kuvuka vikwazo, kinzani na utengano. Jamii ikiendekeza mambo haya, kuna baadhi ya watu wanaweza kutumia mwanya huu kwa ajili ya mafao yao binafsi kwa kutoa majibu rahisi kwa matatizo yanayowakabili wananchi.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya ukweli kwamba, wananchi wa Guinea Conakry kupata bahati ya kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu, bado kuna ugumu wa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya, unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Maaskofu wanapaswa kushikamana na waamini wao ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwani maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika unawategemea hasa waamini walei.

Baba Mtakatifu amewataka Maaskofu kutoka Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanajikita zaidi na zaidi katika kuwajengea uwezo Makatekista ambao ni wadau wakuu wa Uinjilishaji Mpya, ili waweze kutekeleza dhamana yao msingi pamoja na kuendelea kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

Baba Mtakatifu amewaomba Maaskofu kuweka mikakati madhubuti inayopania kuimarisha utume wa Kanisa ndani ya Familia, ili kweli ziwe ni mfano na kielelezo cha kuigwa bila kukanganya mambo. Baba Mtakatifu anasema, utamaduni wa kuoa wake wengi bado unaendelea kushamiri Barani Afrika sanjari na ndoa mchanganyiko.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutoka kifua mbele ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho, tayari kusimama kidete kupambana na baa la umaskini. Hapa kuna haja ya kuendelea kushirikiana na waamini wa dini ya Kiislam, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi nchini Guinea Conakry. Watu wajifunze kuheshimiana na kupokeana hata katika tofauti zao.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza watawa ambao daima wamekuwa karibu sana na wananchi wa Guinea Conakry kutokana na huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Uhaba wa Mapadre, umewafanya hao wachache waliopo kutekeleza utume wao katika mazingira magumu.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kujenga na kuimarisha upendo wa kibaba na urafiki pamoja na Mapadre wao na kwamba Mapadre wanapaswa kuishi na kushuhudia kile wanachokihubiri kwani wao ni kielelezo cha Kanisa mahalia. Baba Mtakatifu anawasihi Maaskofu kujikita katika kuhamasisha miito ya Kipadre na anawapongeza Maaskofu kwa kufungua Seminari iliyopewa jina la Benedikto XVI, ili kutoa fursa kwa Majandokasisi kupata malezi ya kina: kiroho, kimwili na kiutu, tayari kuwatangazia watu Injili ya Furaha inayosimikwa pia katika Mashauri ya Kiinjili. Mapadre watambue vyema utume wao na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu na kwamba, Upadre si ngazi ya kutafutia umaarufu katika Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.