Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai!
Baraza la Maaskofu Katoliki Perù katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa
habari na Malaika kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, sanjari na Siku ya Injili ya Uhai
Duniani, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanaalikwa kusimama kidete kulinda
na kutetea Injili ya Uhai, inayokabiliana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera
za utoaji mimba na kifo laini.
Maaskofu kutoka
Perù wanamwomba Bikira Maria awafundishe kupenda na kuthamini zawadi ya maisha, tangu
pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Familia zijifunze kuwapokea watoto
na hatimaye kuwaonjesha upendo. Wanawake wawe na upendo mkamilifu kwa zawadi ya maisha
wanayoibeba tumboni mwao, wakitambua na kuthamini dhamana na wajibu waliokabidhiwa
na Mwenyezi Mungu wa kutunza zawadi ya uhai tumboni mwao.
Wanawake waguswe
na upendo wa Kikristo na kamwe wasielemewe na: ubinafsi, utamaduni wa kifo pamoja
na kumezwa na malimwengu kiasi cha kuonesha ukatili kwa watoto wao ambao bado hawajazaliwa.
Watoto hawa wana haki zao msingi kama binadamu, kumbe, wasibaguliwe, wasidhalilishwe
wala kubezwa na wale wanaowazunguka.
Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linawaalika
waamini, vyama vya kitume na watetezi wa haki msingi za binadamu kuunga mkono juhudi
za Kanisa katika kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Tarehe 25 Machi, Kanisa linapenda
kuonesha umuhimu wa kulinda na kutetea Injili ya Uhai.
Hii ni fursa makini
ya kutambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu na kwamba, maisha ni zawadi ya Mungu kwa binadamu. Maisha ya mtoto mchanga ambaye
bado yuko tumboni mwa mama yake ni matakatifu, kamwe watu wasithubutu kuyachezea!