Jitahidini kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho wa kweli!
Kuna haja kwa waamini na wananchi wa Senegal katika ujumla wao kuanzisha mchakato
wa umoja, udugu na upatanisho wa kitaifa baada ya watu kupata majeraha makubwa ya
machafuko ya kisiasa nchini humo ambayo yamedumu kwa kitambo kirefu.
Ni ujumbe
wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Senegal, ulioandikwa kwa niaba yake na
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati waamini wa Senegal walipokuwa
wanafanya hija ya ishirini na sita, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Tèmento. Baba
Mtakatifu anasema, wananchi wameathirika sana kutokana na kinzani na migawanyiko,
changamoto ya kuanza ukurasa mpya wa maisha kwa kujikita katika kweli za Kiinjili
na sala bila ya kukata tamaa ili kumwomba Mwenyezi Mungu awawezeshe wananchi wote
kuwa ni vyombo vya amani na upatanisho.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa
Jumapili iliyopita, tarehe 23 Machi 2014 na Askofu mkuu Mariano Montemayor, Balozi
wa Vatican nchini Senegal wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa mahujaji waliokuwa
wamefurika kutoka katika majimbo kadhaa nchini humo.