2014-03-25 09:47:50

Haki, amani, upatanisho, utawala bora na mafao ya wengi ni vipaumbele vya SECAM


Kanisa Barani Afrika litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea: haki na amani; upatanisho, utawala bora na mafao ya wengi. Hivi ni kati ya vipaumbele vilivyofikiwa wakati wa mkutano wa Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Kikanda na Kitaifa, uliokuwa umeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM huko Johannesburg, Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 14 Machi, 2014.

Wakristo wanahamaishwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Maaskofu wao, pamoja na kuwasaidia maboresho ya utume wao kwa kufanya upembuzi yakinifu katika masuala mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa la Mungu Barani Afrika. SECAM inasema kwamba, kwa sasa Kanisa Barani Afrika linapaswa kujikita kwa namna ya pekee kabisa katika mchakato wa kukuza na kuendeleza: haki, amani na upatanisho sanjari na utawala bora.

SECAM inasema, kwamba, kuna haja kwa Wakristo pamoja na watu wenye mapenzi mema kuufanyia kazi ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI, Africae Munus, Dhamana ya Afrika, kwani walengwa wakuu ni Kanisa Barani Afrika. Makatibu wakuu kwa namna ya pekee walipata nafasi ya kutafakari kuhusu machafuko ya kisiasa uanayoendelea sehemu mbali mbali Barani Afrika, lakini kwa namna ya pekee katika Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Sudan ya Kusini.

Wanasema, umefika wakati kwa wanasiasa kuachana na falsafa ya vita na kujikita katika majadiliano yanayozingatia, ukweli, amani na mafao ya wengi. Vita itaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.