2014-03-24 09:06:58

Upendo na huruma ya Mungu ina nguvu ya kuvuka mawazo mabaya!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresma inamwonesha Yesu akizungumza na mwanamke Msamaria, mazungumzo ambayo yalisaidia kuvunjilia mbali uhasama na chuki iliyokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria, kiasi hata cha kuweza kupenya katika undani wa maisha ya mwanamke Msamaria. Yesu anafanya yote haya bila wasi wasi wala woga, anakutana na mwanamke ambaye anapenda kumwonjesha upendo wa dhati, unaoleta mabadiliko ya ndani kwa kuvuka mawazo mabaya kwa kukumbatia uhalisia wa maisha!

Ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uliokuwa umefurika kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili tarehe 23 Machi 2014. Yesu alimwomba mwanamke Msamaria maji ya kunywa ili kuamsha ndani mwake ile kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo kiu ambayo iko katika maisha ya mwanadamu, lakini kwa bahati mbaya, watu wengi bado hawajapata ujasiri wa kujadiliana na Yesu, kwa kuangalia undani wa maisha yao, anasema Baba Mtakatifu Francisko! Mwanamke Msamaria ni changamoto kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili hatimaye, kuwa na ujasiri wa kumwomba Yesu maji yatakayozima kiu ya maisha ya uzima wa milele!

Mitume wa Yesu waliporejea kutoka mjini, walishangaa kumwona Yesu akizungumza na Mwanamke Msamaria, lakini Baba Mtakatifu anasema, huruma na upendo wa Mungu ni mkuu unashinda mawazo potofu! Yesu ameonesha kwamba, ni chemchemi ya huruma kwa watu wote wanaomkimbilia. Mwanamke Msamaria anaonja nguvu ya upendo inayomletea mabadiliko ya ndani, kiasi cha kukimbia na kwenda kuwatangazia watu matendo makuu ya Mungu yaliyomwezesha kupata maji ya uzima wa milele, maji ambayo alikuwa anayatafuta kwa udi na uvumba!

Mwanamke Msamaria anakwenda Kijijini kwake, kule ambako watu wengi walikuwa wanamwangalia kwa "jicho la kengeza" kutokana na maisha yake, lakini aliwatangazia kwamba, amekutana na Masiha aliyemwonesha mwelekeo mpya wa maisha. Kila mara mwamini anapokutana na Yesu, maisha yake yanabadilika, anasema Baba Mtakatifu, changamoto ya kukimbilia upendo wa Mungu, ili kugundua maana ya maisha ya Kikristo yanayopata chimbuko lake kutoka katika Kisima cha Ubatizo.

Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Yesu anayebadili mwelekeo wa maisha yao, kiasi cha kuwawezesha kuwamegea wengine ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao!

Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka wagonjwa wa Kifua Kikuu, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu, tarehe 24 Machi, 2014. Amezungumzia pia Siku kuu ya Upatanisho, itakayoadhimishwa hapo tarehe 28 Machi 2014 kwa Makanisa kuwa wazi ili kutoa fursa kwa waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.