Kila siku Kanisa hukumbuka Fumbo la kuzaliwa Bwana linaposali Sala ya Malaika wa Bwana.
Bikira Maria alikubali kuwa ni Mama wa Mungu, baada ya kusikia wito kutoka kwa Mwenyezi
Mungu kwa njia ya Malaika Gabrieli. Tangu wakati huo Bikira Maria akawa ni Tabernakulo
ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Hii ni Sherehe inayoadhimishwa na Mama
Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Machi.
Kwa mwaka
huu Sherehe hii ina uzito wa pekee Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sinodi maalum
ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ili kuweza kukabiliana na changamoto za kichungaji
zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Familia sehemu mbali mbali za dunia.
Katika Maadhimisho ya Sherehe hii sanjari na Siku ya kuenzi Uhai, Baraza la
Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake kwa waamini na watu wenye mapenzi mema
katika Siku ya Kuenzi Uhai, linawataka waamini kusimama kidete kuenzi Injili ya Uhai,
chemchemi ya matumaini mapya katika kipindi cha myumbo wa uchumi kimataifa. Maaskofu
wanaialika Familia ya Mungu nchini Hispania kukumbatia Injili ya Uhai na kuachana
na utamaduni wa kifo, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Hispania, Ulaya na dunia katika
ujumla wake.
Hii ni dhamana inayowawajibisha kimaadili kupokea na kuikumbatia
zawadi ya uhai kwani ni rasilimali kubwa katika kuleta mabadiliko katika sekta mbali
mbali za maisha ya mwanadamu. Mataifa makubwa yaliyokuwa yameaathirika kutokana na
maafa mbali mbali yaliweza kusimama tena kwa kutumia rasilimali watu, iliyokuwepo.
Hii ndiyo nguvu kazi iliyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya mataifa haya.
Maaskofu wanasema, Hispania inakabiliwa na idadi
ndogo sana ya watoto wanaozaliwa, hali inayotia wasi wasi kwa ajili ya ustai wa Jamii
kwa siku za usoni. Kumbe kuna haja ya kuwa na mpango mkakati wa kiuchumi, kijamii
na maisha ya kiroho kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutambua na kuenzi zawadi ya
ndoa na maisha ya kifamilia. Serikali na wadau mbali mbali hawana budi kupanga sera
na mikakati itakayoziwezesha Familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.
Maaskofu
wanasema, jambo la msingi zaidi ni watu kubadili mtazamo na mtindo wa maisha kwa kujikita
katika uhuru unaowajibisha kwa kuwahamasisha kujitoa kwa ajili ya maisha ya ndoa na
familia katika upendo wa dhati. Hii nichangamoto kwa familia kuoneshana na kumegeana
upendo kati yao na wale wote wanaowazunguka. Hivi ndivyo anavyoendelea kukazia Baba
Mtakatifu Francisko kwa watu wa ndoa na familia.
Ikiwa kama Jamii itashindwa
kuwasaidia watoto na wazee, haina mizizi ya matumaini kwa siku za usoni. Utu na heshima
ya binadamu inapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa
mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa
Mungu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika waamini na watu wote
wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu familia kama chemchemi ya matumaini
mapya, changamoto na mwaliko wa kupokea kwa imani na matumaini zawadi ya maisha.
Waamini
na watu wote wenye mapenzi mema, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kusimama kidete
kulinda na kutetea Injili ya Uhai, dhidi ya majanga ya kiuchumi na kijamii yanayoweza
kujitokeza kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Watoto na vijana wa kizazi kipya wanazungukwa
na mambo mengi ambayo yanawakatisha tamaa hata kuweza kufanya maamuzi magumu siku
za usoni, lakini Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika kugundua zawadi
ya uhai kama chemchemi ya matumaini mapya.
Imehaririwa na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.