Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 22 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao wamelipongeza
Kanisa kutokana na mchango wake wa hali na mali katika sekta ya elimu, afya na maendeleo
endelevu ya wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.
Wamekazia umuhimu wa kukuza
na kuendeleza majadiliano ya kina kati ya makundi mbali mbali nchini Nigeria kwa ajili
ya kudumisha haki, amani na upatanisho wakitaifa. Viongozi hao wamekazia kwa namna
ya pekee kabisa umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, haki msingi za
binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu. Wamelaani vitendo vya mauaji ya watu wasiokuwa
na hatia vinavyoendelea kushamiri nchini Nigeria kila kukicha!
Rais Jonathan
na ujumbe wake walikutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu
wa Vatican aliyeambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya
nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Askofu mkuu Ignatius
Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, amesema kwamba, kwa sasa
wananchi wa Nigeria wamechoshwa kusikia mabadiliko ya mbinu mkakati wa kupambana na
kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, kwani kwa sasa wanataka kuona vitendo kwamba,
magaidi wanashughulikiwa kikamilifu kisheria. Mkakati huu hauna budi kwenda sanjari
na maboresho ya sera na vipaumbele katika masuala ya maendeleo ya watu kiuchumi na
kijamii, ili kukidhi mahitaji msingi ya watu katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria.
Nigeria
kwa sasa imezindua mbinu mkakati mpya ambao umeandaliwa katika kipindi cha mwaka mmoja
na nusu uliopita, kwa kushirikiana na “nguri” kutoka mataifa mbali mbali katika kupambana
na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ambacho kwa sasa kimekuwa nitishio kubwa kwa
watu na mali zao nchini Nigeria. Utekelezaji wa mkakati huu hauna budi kufanyika mapema
iwezekanavyo kwani, mambo yanazidi kuwa magumu kila kukicha anasema Askofu mkuu Kaigama.
Wananchi wengi wa Nigeria wanataka kuona amani na utulivu, usawa na utawala
wa sheria ukishika mkondo wake. Kanisa linaendelea kusali ili kweli amani na utulivu
viweze kurudi tena nchini Nigeria.