Wanawake waandamana Msumbiji kupinga ndoa na watesi wao!
Hivi karibuni, maelfu ya wanawake na wasichana nchini Msumbiji wamefanya maandamano
makubwa mjini Maputo kupinga muswada wa sheria unaowataka wanawake waliobakwa na kunyanyaswa
na wanaume kuolewa nao kwa walau kipindi cha miaka minne badala ya kufungwa gerezani.
Wanawake na pamoja na wanaharakati wanasema, muswada huu wa sheria una mapungufu
makubwa kwani unakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu na kwamba, unapaswa kufanyiwa
marekebisho makubwa, ili watuhumiwa wanaoendekeza vitendo vya kuwanyanyasa wanawake
na wasichana wanapopatikana na hatia, sheria ishike mkondo wake, kama fundisho kwa
wote wanaoendekeza mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.
Kimsingi muswada
wa sheria hii unapata chimbuko lake katika sheria za Msumbiji za Mwaka 1886 zilizoachwa
na Wareno wakati wanatawala Msumbiji. Kadiri ya mila na tamaduni za Msumbiji, ndoa
za namna hii bado zinakubalika, lakini wanawake na wanaharaki wanasema, umefika wakati
kwa Msumbiji kufanya mabadiliko makubwa ili kutetea utu na heshima ya wanawake wa
Msumbiji.
Muswada huu wa sheria unataka kuendekeza bado mfumo dume unaowakandamiza
na kuwanyanyasa wanawake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.