Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania kwa Bunge
Maalum la Katiba linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma, tarehe 21 Machi 2014.
Ameichambua rasimu ya katiba, ameonesha ugumu na changamoto zinazopaswa kufanyiwa
kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Wabunge hawa wanapaswa kuongozwa
na kauli mbi "Tanzania Kwanza".
Pongezi Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe
wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu.
Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za
Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa
na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania. Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili
maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha cha imani kubwa
na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania
wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa
jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge
Maalum la Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi
yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa
kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi. Katiba inayotekelezeka.
Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba
itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha
umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha
ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia,
rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama
na utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala
wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu. Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa
umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi
wengi kunufaika sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe; Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa
kutunga Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda
na mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti
na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio
watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia
walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu
ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba
ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu
na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo, kwa Katiba
zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum.
Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na
wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya
Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura
ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato
iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tangu kutungwa
kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au
kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali
hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa ruksa yako naomba nitaje
baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:- 1. Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama
ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada
ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
2. Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu
Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
3. Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla
ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara
ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine
ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4.
Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa badala
ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na
Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu
wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia
15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge
lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
5.
Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea
Mwenza.
6. Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko
yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu
wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kufanyika kwa mabadiliko
hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa
kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo
na madai yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa
kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa
sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai
Katiba mpya kwa imani, eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu,
hata katika mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika
kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi
wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa kutambua ukweli huo
na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala
na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira
ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato
huo tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia,
dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika
pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya Mheshimiwa
Mwenyekiti; Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu
wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja
mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe
Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum
la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa
wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na kuikamilisha
kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar,
Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti
wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu
tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada
ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga
kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Rasimu ya Katiba ilichapishwa
kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa
katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa
ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma.
Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na
kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni
yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo
thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania
wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi
kwa Tume Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi
za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa
Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa
na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu,
wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu
Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja
na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na
kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika,
walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada
ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao,
Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko
mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa
Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha
taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza
Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume imefanya
kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa
vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa
yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka
msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba
tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe
Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura
17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa
ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini
mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata
neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba
na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa
au kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya
hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa
na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe
marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia
balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika mchakato
huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika
hatua moja kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo
muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Nimekwishaeleza kuwa
moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba
ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi
ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya
Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa
(too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika
Katiba bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako
mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda
mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba
ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili.
Simaanishi kwamba tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa
au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine ambayo
haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba
ambayo ni ngumu kutekeleza. Mheshimiwa Mwenyekiti; Yapo pia maoni kuwa baadhi
ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho.
Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano,
Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka
kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha
sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi
kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa
utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni
jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo
la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano
ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo
ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo
yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa
na Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji,
uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako chini
ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano ni kwa
mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama
wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili
wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo
ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali
ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati
ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu
muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala haina
uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka
ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya
mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa
Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu.
Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya Mheshimiwa
Mwenyekiti; Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo
yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake
na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji
mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu
wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie baadhi ya dhana na mambo
mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d)
inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge
kwa miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu
hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani
na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa.
Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo
hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo
cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna
haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa
na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge
kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni
ukatili ambao haustahili kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine
Mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa
miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika mwisho. Kwa
nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti
hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi?
Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike
ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi
cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo hili mkalitazama kwa
makini, na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena
mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala
motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa
ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo
kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo
Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana
na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu
mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu
za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine jipya linalopendekezwa
na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa
hoja linaonekana kuwa jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna
hatari ya kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao
kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa.
Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika
mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa
Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba wenzao
mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani inayoongezwa na kuanzisha
utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi
kila miaka mitano kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine
kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu wote nchini linahusu
muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo
hili limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa
katika Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa
kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa
sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu.
Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi
wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni
jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo
hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa
nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi
ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe; Kama alivyoeleza
Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai
ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo
ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya
hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya
Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji
Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika
wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa
sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika;
na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika
na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Natambua kuwepo kwa rai
ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo mimi ni vigumu kuacha
kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa
mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu.
Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa.
Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki
mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni
kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili
muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama
zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko.
(you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume imetoa
sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu ya kwanza ni kwamba
ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi
kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga
mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga
mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu
ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa
na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana
na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania
wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki.
Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe. Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa taarifa
ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi
walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa
na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia
86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.
Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa
ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti; Wanasema pia, kwamba
mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati
ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa
na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka
Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza
Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti; Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile
kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia
muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera
Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi
ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa
asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa
asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania
wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali
Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe; Kama nilivyokwishagusia
awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa muundo wa Serikali tatu
ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha
vizuri changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia
kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo
kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar
hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano,
na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia
mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia
Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Aidha,
kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka
1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Kwa upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko
kuwa Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika
na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano.
Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na
Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi
na kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge lazima
zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika Zanzibar. Wananchi
wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati
wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia
mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi
ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili
muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida
za Muundo wa Serikali Tatu Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati ya
mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho
wao wa kihistoria na kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa
na Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya
Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo
baina ya washirika na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida
za Muundo wa Serikali Mbili Mheshimiwa Mwenyekiti; Pamoja na kuainisha
changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo wa Serikali tatu
ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa
na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili
unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano na
ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za
Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa
ulipo tangu kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia
kudumisha amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali
Tatu Mheshimiwa Mwenyekiti; Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali
tatu kama jawabu kwa changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu
nao una changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na
gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa
hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti. Alisema
kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa
ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa
ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba
katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama za
uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna uwezekano
wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua
mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya Muungano.
Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya
pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano. Muundo huu pia unaweza
kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision making) katika kufanya uamuzi
juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa
ustawi wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali
tatu kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue
Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza
matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri
kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza
kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa
mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika
kipindi cha uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero
za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na Kamati
ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume
ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande
wa kero zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia
mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati
ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi
ya kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni: 1.
Mgawanyo wa mapato: (a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika
Mashariki (b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu. 2.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili. 3. Ushirikiano wa Zanzibar na
taasisi za nje. 4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano. 5.
Usajili wa vyombo vya moto. 6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu
wa mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo: 1. Utafutaji na uchimbaji
mafuta na gesi asili. 2. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje. 3.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za
kiutawala. Hali kadhalika, katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani
2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba
ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile
tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa tofauti
zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano Mheshimiwa Mwenyekiti; Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi wala
upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza
kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano kutaka
kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala siyo udhaifu wa
viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa
na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za Muungano.
Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki
za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa
uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura
za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano,
ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate
kujua ukweli na undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mambo hayo ni haya yafuatayo: 1. Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 2.
Mambo ya Nje, 3. Ulinzi, 4. Polisi, 5. Hali ya Hatari, 6.
Uraia, 7. Uhamiaji, 8. Biashara ya nje na mikopo, 9. Utumishi
katika Serikali ya Muungano, 10. Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa
Forodha na Ushuru wa Bidhaa, 11. Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11
hadi kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye
ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana kuwa
mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa.
Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha
mabadiliko hayo kufanywa.
Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa
ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia
kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka
1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu
yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu
mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada
husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu
Urais tarehe 10 Juni, 1965.
2. Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa
mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:- (a) Leseni za Viwanda
na Takwimu, (Jambo la 13) (b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14) (c) Jambo la
15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa
jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki,
Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara,
Usafiri wa Majini na kadhalika.
3. Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali
ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na
kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta
ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha
ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
4.
Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16.
Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo
nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
5.
Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya
Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano
yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji
wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na
Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
6. Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa”
na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa
kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote
ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo
mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila yalipotokea
mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa
zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo
wake mkubwa wa kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande kushughulikia
ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na uamuzi wetu wenyewe
ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji
wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti; Ni msimamo wa Serikali
zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano
ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za
Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni
za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa
miaka kadhaa sasa na imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia
fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo tutakayokubaliana
kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi
Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa
suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili
tulishakubaliana tangu wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja
Rais Shein msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa fikra
za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria
wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa
ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya “subira yavuta
heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo
sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo
ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa
na makampuni binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar
ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki,
mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa
upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar
na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine muhimu
ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu
Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada
kutoka nchi za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali.
Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hisia
hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali
ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania
Bara imejificha kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili
iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar.
Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa
kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana
kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana
iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana,
itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au
taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa
mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa
hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu.
Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa maoni yangu kitu kingine
muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha
inatimiza ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe
ipasavyo kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya
kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya
Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano
na ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana
budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo yote sawa
hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Waheshimiwa
Wajumbe; Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye
Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto
za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya
watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba
myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza,
kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye
msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi
washirika. Kwa sababu hiyo inaweza kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika,
iwapo itakosa ihsani ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja
wa washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo
cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake.
Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia,
kwamba, hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina
chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama
wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa
kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina
uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina
mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo.
Katika mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza
majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa
kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa sababu ya
kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka.
Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine
wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika
akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo
cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli
uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu
hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa,
zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa
iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea.
Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo
bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza
kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa
nguzo ya kutegemewa na nchi washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo
huo linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili
wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto
za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika kuainisha changamoto
za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili
makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo
ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya
uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic
sentiments) wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo
haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano,
bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi
ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa
Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Ni lazima lifanyike kila
linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani yakikwama maana yake shughuli
za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano
utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika.
Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika,
yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria,
watu walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi
moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika
na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita takriban
asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua
ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika,
watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri
na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na
fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara moja
watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili
ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora waondoke.
Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma
maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa
Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta
watu wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012
na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar,
huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na
kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali
zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne,
ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka
na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna budi
kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio sahihi. Tusije tukajutia
uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia
hatua hiyo Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu. Kwa kweli, unapoyatafakari
haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi waliamua walivyoamua. Waliona
mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza
kila kitu tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa
hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993
alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu…
na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti; Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza:
“Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo
yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu atachukua njia
yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa
matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi
Yenu Kubwa Mheshimiwa Mwenyekiti; Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini
kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona
katika kuipitia Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe
la kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa
vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili,
ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili
hiyo, ni muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni
muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi
ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na Watanzania wote kupata
Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12
wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya
watu wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa
ya kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa.
Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote mtakuwa
mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea
kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume
chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda Mheshimiwa Mwenyekiti; Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa
na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti
wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na
ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu
sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa
kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel
Sitta.
Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo
hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa
kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao kwenu. Hamna budi,
haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa
lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili,
baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea
kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye
vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali
ile haitajirudia tena katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata
tamaa na Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa
nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna
haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana
ngumi, kutishiana hili na lile au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa
kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni
Maslahi ya Taifa Mbele Mheshimiwa Mwenyekiti; Ombi langu la mwisho kwenu
ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali maslahi mapana ya nchi yetu na watu
wake badala ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu
iwe “Tanzania Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo
kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi
yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo na
mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa
tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo
wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari
kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni
kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu usiokubaliana
nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe; Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya
kulazimisha. Mkifanya hivyo hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna
ya kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna
ya kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana, hili ni
jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote
washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa
na asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano,
mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri
katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo, tafadhalini zitumieni.
Jengeni madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini
tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende salama.
Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa
kwa taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada ya kusema maneno yangu mengi
hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia
Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Libariki
Bunge Maalumu la Katiba! Asanteni sana kwa kunisikiliza!