2014-03-22 08:47:37

Miaka 30 ya Uaskofu, Miaka 43 ya Upadre na Miaka 16 ya Ukardinali! Hongera Kardinali Pengo


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatfu Yosefu, Mchumba wa Bikira Maria na Msimamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ameadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu, Miaka 43 ya Upadre na Miaka 16 tangu alipoteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kuwa Kardinali wa pili kutoka Tanzania, muda mfupi tu baada ya kufariki kwa Kardinali Laurean Rugambwa.

Kardinali Pengo alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 huko Mwanzye, Sumbawanga na baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 20 Juni 1971. Kunako tarehe 11 Novemba 1983 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Nachingwea lililobadilishwa na kuwa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi. Tarehe 22 Januari 1990 aliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tarehe 22 Julai 1992 akawa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam baada ya Kardinali Rugambwa kung'atuka kutoka madarakani. Tarehe 18 Januari 1998 akateuliwa kuwa Kardinali.

Katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Pengo ametoa shukrani zake za dhati kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam na Tanzania katika ujumla wake kwa kumwonesha moyo wa upendo, umoja na mshikamano wa kidugu katika utekelezaji wa dhamana yake ndani ya Kanisa. Kardinali Pengo anasema, alipoingia Jimbo kuu la Dar es Salaam, kulikuwa na Parokia 20 ambazo nyingi zilikuwa zinaongozwa na Wamissionari, leo hii, kuna jumla ya Parokia 79.

Kardinali Pengo anasema, ndoto yake ni kuhakikisha kwamba, kabla ya Mwenyezi Mungu hajamwita mbele ya haki, awe tayari amekwisha anzisha Parokia 100 kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ndoto inayoweza kufikiwa tu, kwa njia ya ushirikiano wa dhati na Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amewataka waamini kuwa wasikivu kwa sauti ya Mungu inayowaita kila mmoja katika maisha na utume wake. Waamini watambue fika na wala wasibabaishe kuhusu wito wao kama ni ndoa, utawa na maisha ya kipadre, daima wawe tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kila mwamini anapaswa kuwa imara katika maisha na wito wake.

Akizungumza katika Ibada hiyo, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania anasema, Kardinali Pengo aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea akiwa na kijana mbichi, lakini mnyenyekevu katika kuwahudumia Watu wa Mungu. Amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumsindikiza Kardinali Polycarp Pengo katika maisha na utume wake, kama ilivyo kawaida yake, kwa kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza Jimbo kuu la Dar es Salaam na Tanzania katika ujumla wake, kwa imani, matumaini na moyo mkuu.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amempongeza Kardinali Pengo kwa moyo wa ushirikiano na Maaskofu Katoliki Tanzania. Familia ya Mungu nchini Tanzania ina mshukuru Mungu kwa zawadi ya Kardinali Pengo kwa kuwaongoza Watu wa Mungu kwa moyo wa unyenyekevu, upendo, majitoleo na sadaka kubwa. Ameitaka Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuendelea kumpatia ushirikiano na mshikamano wa dhati Kardinali Pengo katika utekelezaji wa majukumu yake ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kwa niaba ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, Askofu mkuu Tarcisio Zizaye, Mwenyekiti wa AMECEA anasema, Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA, inampongeza Kardinali Pengo kutokana na mchango wake mkubwa si tu kwa Kanisa la Tanzania na Afrika bali hata kwa Kanisa la Kiulimwengu. AMECEA inamwombea kheri na baraka tele katika maisha na utume wake wa: kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha Watu wa Mungu kwa upendo na moyo mkuu. Ujumbe kutoka AMECEA umeandikwa na Padre Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa AMECEA.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.