2014-03-21 07:29:29

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, tuko tayari Dominika ya III ya Kwaresima kipindi maalum katika mwaka wa Liturujia kwa ajili ya kujitakatifuza zaidi pamoja na kuyatakatifuza malimwengu. RealAudioMP3
Neno la Mungu latualika kutambua zawadi mpya za kimungu. Tunasikia katika somo la kwanza safari ya Waisraeli toka Misri. Wamekwishavuka Bahari ya Shamu na wanaelekea nchi ya ahadi. Katika simulizi hilo inaonekana kwamba hapo mwanzoni hali ilikuwa nzuri na waliona kila kitu kinaongozwa na Mungu, lakini baadaye ilianza kubadilika na hivi mapungufu ya mahitaji yakaanza kujitokeza, wanakutana na nyoka, joto nk.

Leo tunasikia shida ya maji, ambayo sasa inajitokeza kwa malalamiko kinyume na Musa. Wanaona Mungu hawasaidii hata kidogo, amepoteza uaminifu wake na hivi pengine alitaka kuwapeleka katika kifo badala ya kuwapeleka katika nchi yao!

Mpendwa mwana wa Mungu, Waisraeli wanajiuliza maswali kadhaa: hivi Mungu yu hai, hivi Mungu yu pamoja nasi au hapana? Basi tokana na maswali haya yaliyojaa majadiliano, sehemu yalipofanyika panaitwa Masa na Meriba jangwani wakilishi Kishawishi.

Mpendwa msikilizaji, shida na malalamiko yanayowagusa wana wa Israeli hayako mbali nasi. Tulipopokea ubatizo au ndoa au upadre mambo yalikuwa safi, furaha tele na shangwe, lakini polepole tunapokabiliana na majukumu na haki kuhusu sakramenti hizi huanza kujitokeza magumu na misalaba na kama hatuko makini malalamiko huanza na hata kinyume na Mungu. Basi kwaresima hii ni kusali kuomba ili tupate kutunza upole na uvumilivu wa moyo. Mkristu anavumilia mpaka Kalvari, hakuna kurudi nyuma kamwe.

Mt. Paulo anapowaandikia Warumi na hivi kutuandikia sisi hivi leo, anakazia tumaini lililojisimika katika mapendo ya Mungu kwetu pasipo kutegemea udhaifu wetu au wema wetu bali ni mkamilifu siku zote. Ndiyo kusema upendo wake haute gemei kazi nzuri tunazofanya. Mungu huwapenda hata adui zake, kinyume nasi ambao mwelekeo wetu ni kuwachukia adui zetu. Basi katika kwaresima hii tufunge ili tuweze kufungua macho ya mapendo kwa wote kama ambavyo mwanga ni kwa wote.

Katika Injili tunakutana na picha ya mwanamke msamaria aliyekutana na Masiha katika kile kinachoitwa kisima cha Yakobo. Katika mantiki ya wakati ule kisimani palikuwa ni sehemu ya wanakijiji kukutana. Wachungaji walifika pale kwa ajili ya kunywesha mifugo yao. Wafanyabiashara walikutana na wanunuaji wa mali zao. Si haya tu bali pia akina mama walikwenda kuteka maji kwa ajili ya familia zao. Injili ya leo inachukua sehemu mojawapo ya mikutano mbalimbali kama tulivyokwisha itaja. Bwana anakutana na mwanamke Msamaria aliyekuja kuteka maji.

Yesu alikuwa amechoka kwa safari na alikuwa anapumzika pale akiwasubiri Mitume waliokuwa wamekwenda mjini kununua chakula. Kwa vyovyote vile Bwana hakuwa na kichoteo kwa ajili ya kuchukua maji na kunywa na kwa kuwa kisima kilikuwa kirefu yapata meta 32 hivi asingeweza bila kichoteo. Basi anaomba msaada toka kwa mama msamaria. Mara moja mama huyu atagundua, nadhani kwa sauti kuwa huyu ni mgalilaya!

Mpendwa msikilizaji, katika hili, kinachofuata ni maswali: hivi inawezekanaje mgalilaya akaomba msaada kwa msamaria? Ni kwa uwezo gani mtu huyu aweza kuvunja mila ambayo hairuhusu mwanamme akiwa peke yake kuongea na mwanamke asiyemfahamu? Katika hili sheria yao iliruhusu kuongea maneno machache wakati mtu anahitaji maelekezo fulani! Hata hivyo, Bwana anavunja miiko hii, akitaka kuondoa utengano uliojikita katika mila na desturi. Anachotafuta ni usafi wa moyo na si wasiwasi na mashaka ya nje.

Mpendwa msikilizaji, kitendo cha Bwana kukutana na mwanamke msamaria pale kisimani katika Injili ya Matayo kinatupa tafakari ya ndani kabisa. Kisima ni sehemu ya makutano ya wachumba ambao baadaye wataoana. Katika Agano la Kale taifa la Israeli lilitambuliwa kama mchumba wa Mungu. Lakini tukisonga mbele, tunaona jinsi mchumba Israeli alivyovunja agano na Mungu, na hasa anapomsaliti mchumba wake wa kwanza na kuanza kwenda kwa wachumba wengine: Wamisri, Waasiria, Wababilonia, Wapersia na mwishoni Warumi!!

Basi tunaporudi katika Injili ya leo tunakutana na huyu mama msamaria ambaye yuko pale kuwakilisha taifa la Israeli ambalo halikuwa aminifu mbele ya Agano na Mungu. Kwa hakika mama huyu alikuwa malaya. Kumbe Bwana anapokutana naye anataka kumrudisha katika pendo la Mungu, anataka arudi katika uhuru kamili na ajipatie heshima yake aliyoipoteza katika jumuiya. Je, sisi tuko mbali na mambo haya? Tutafakari!

Mpendwa msikilizaji, Bwana anataka kumpatia mama huyu chakula na maji yakatayo kiu daima na wala si maji ya kisima kile cha Yakobo. Maji ya kisima cha Yakobo ni ishara ya mambo yote mtu ayatafutayo akifikiri yatamaliza kiu yake na badala yake huiongeza na hata kukata tamaa. Mpendwa jaribu kufikiri unapotenda dhambi ukifikiri itakupa furaha, baada ya muda unaanza kurudi nyuma na kujiuliza maswali kadhaa: hivi kwa nini nimefanya jambo hili, Je ningekamatwa?, Basi shida na msongo wa maswali huendelea mpaka pale tu utakapoondolewa dhambi hiyo na ndipo utatulia. Mpendwa msikilizaji katika hili kumbuka utulivu na furaha vinapatikana katika kutimiza mapenzi ya Mungu tu. (Roho yangu haitulii mpaka hapo itakapotulia katika Mungu, Mtakatifu Agustino wa Hipo).

Mpendwa mwana wa Mungu, Bwana anapendekeza na kutoa maji mapya yakatayo kiu daima, nayo ni roho ya Mungu, ndiyo usema anayejikabidhi kuongozwa na roho wa Mungu atapata utulivu na furaha moyoni na maishani mwake. Mama msamaria anakuwa mfano wa ukuaji wa kiroho, maana mwanzoni alimwona Bwana kama msafiri na kisha akawa Bwana, polepole Nabii, Masiha na mwishoni ni Mkombozi wa ulimwengu. Nasi wapendwa kukutana na Mungu kwa njia ya Neno lake au jumuiya Kanisa, kunatupasa kutufanya tukue kiroho na kuanza maisha mapya. Mwanamke msamaria anaacha mara moja mtungi wa maji baada ya kutambua Masiha na anakwenda kutangaza habari njema hiyo, habari ya furaha. Ni wajibu uleule tunaopaswa kuutenda mara tu tunapogundua nani ni Masiha yaani, aliyekuja kuleta uhuru na kukarabati upendo msingi uliokusudiwa tangu kuumbwa ulimwengu.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, ninakutakia furaha na matumaini katika maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa namna hiyo kuijua hekima ya kweli itokayo kwa Mungu aliye kisima kipya cha wokovu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.