Mwanasheria mkuu mstaafu wa Kenya, Amos Wako amewawaonya Wabunge wa Bunge Maalum la
Katiba linaloendelea nchini Tanzania kuwa makini na wala wasikubali kuiga mambo ya
Katiba za nchi nyingine bila kuangalia uhalisia wa maisha na mazingira ya watanzania
wenyewe. Wabunge wazingatie kwanza kabisa haki msingi za binadamu, umoja wa kitaifa,
ustawi na mafao ya watanzania wengi.
Amos Wako ameyasema hayo wakati alipokuwa
anashirikisha mang'amuzi ya mchakato wa utungaji wa Katiba Mpya ya Kenya miaka kadhaa
iliyopita. Anasema, mchakato wa Katiba Mpya nchini Tanzania unaendelea vyema na kwamba,
unawashirikisha watu kutoka katika makundi mbali mbali na baadaye Watanzania watapata
fursa ya kuupigia kura ya maoni, kuukubali muswada au kuukataa. Kumbe, ni vyema wabunge
hao wakatumia vyema dhamana waliyokabidhwa na watanzania wenzao ili kuweza kupata
Katiba bora zaidi ambayo kimsingi ni Sheria Mama.
Amewaomba Wabunge kuzingatia
misingi ya haki, amani na utulivu; kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini
na kupingana kwa nguvu ya hoja, kwa ajili ya mafao na ustawi wa watanzania. Wabunge
wasikubali kushindwa na kishawishi kitakachowatumbukiza katika machafuko ya kisiasa
kama ilivyojitokeza katika sehemu mbali mbali za dunia wakati wa mchakato wa kuandika
Katiba Mpya. Wajitahidi kuhakikisha kwamba, Katiba Mpya inakuwa ni Mali ya Wananchi
kwa kuwahusisha wananchi wenyewe. Mchakato wa kupata viongozi watendaji wakuu wa Serikali
umebainishwa vyema katika Mchakato wa Katiba, hali inayoonesha umuhimu wa kukuza na
kudumisha misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji.