Mwezi Novemba 2012 Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilianzisha Siku ya Misitu Duniani,
inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 21 Machi. Lengo ni kuwahamasisha watu kulinda,
kutunza na kuendeleza misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika ujumbe wake kwa Siku hii, inaitaka
Jumuiya ya Kimataifa kulinda misitu kwani ni kikolezo kikubwa cha maendeleo ya mwanadamu
sanjari na mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa usalama wa chakula duniani. Utunzaji
bora wa misitu unaweza kusaidia kudhibiti kwa kiasi kikubwa madhara yanayosababishwa
na mabadiliko ya tabianchi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba,
zaidi ya watu billioni 1.6 wanategemea misitu kwa ajili ya kupata chakula, nishati,
makazi na pato katika maisha. Takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO, zinaonesha
kwamba, watu asilimia 65% hadi 80% wanategemea dawa zitokanazo na misitu kama chanzo
cha tiba kwa magonjwa yanayowasibu.
Misitu ni kikolezo kikubwa cha maendeleo
endelevu katika viwango mbali mbali na inachangia walau asilimi 1% ya Pato Ghafi la
Taifa na kwamba, misitu ni mhimili mkubwa katika sekta ya kilimo, viwanda, nishati
na matumizi ya nyumbani. Umoja wa Mataifa unawataka wadau mbali mbali kuhakikisha
kwamba, wanatumia siku hii kwa ajili ya kuhamasisha watu juu ya utunzaji bora wa misitu
kwa ajili ya mafao ya wengi.