Mjadala wa kuruhusu matumizi haramu ya dawa za kulevya ni kwa mafao ya nani?
Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya iliyopewa dhamana ya kuhakikisha kwamba,
itifaki zilizoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa kuhusu udhibiti wa dawa za kulevya unatekelezwa
katika ni jambo la msingi sana.
Haya yamo
katika taarifa yake inayohusu Hali ya Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa kwa Mwaka
2013, inaonesha madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya katika: uchumi na jamii;
afya na usalama wa raia; uhalifu na vitendo vya jinai, tija na uzalishaji pamoja na
utawala bora.
Bodi hii imeonesha msimamo wake kwa kutokubaliana na maamuzi
yanayotolewa na baadhi ya nchi duniani kwa kutaka kuruhusu matumizi ya dawa za kulevya,
kama ilivyojitokeza hivi karibuni nchini Uruguay na katika baadhi ya majimbo nchini
Marekani. Baadhi ya watu wanaounga mkono mwelekeo huu mpya wanasema kwamba, gharama
ya kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya ni kubwa mno na ina hatari kubwa.
Bodi
ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya inasema kwamba, hoja hii haina nguvu kwani
Serikali nyingi zinaendelea kupata kodi kubwa kwa kuuza vileo na tumbaku, lakini gharama
ya afya inayotokana na matumizi ya vileo na tumbaku ni kubwa mno ikilinganishwa na
kodi inayolipwa kwa serikali.
Ikiwa kama Serikali mbali mbali duniani zitaendelea
kuruhusu matumizi haramu ya dawa za kulevya. Itabidi pia kuongeza nguvu katika mchakato
wa ulinzi na usalama, kwani takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba, watu wengi waliofikishwa
kwenye mkondo wa sheria ni wale ambao wamekutwa na makosa yanayohusiana na ulevi pamoja
na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Baadhi ya hoja zinazotolewa ni kwamba,
ikiwa kama matumizi ya dawa za kulevya yataruhusiwa, wafanyabishara waliokuwa wanategemea
sana biashara hii kama chanzo cha pato lao watakamwa. Lakini, Bodi ya Kimataifa inasema,
hoja hii haina nguvu kwani wafanyabiashara wa dawa haramu za kulevya wanaweza kuingia
katika soko halali la dawa za kulevya pamoja na kuendeleza soko haramu la dawa hizi
kama ilivyo katika biashara ya sigara duniani. Asilimia 9% hadi 20% ya Soko la Sigara
Uingereza inatokana na biashara ya magendo ya sigara na hivyo wanaikosesha Serikali
kodi halali wanayopaswa kulipa.
Takwimu za Kimataifa zinaonesha kwamba, kumekuwepo
na ongezeko kubwa la ajali barabarani zinazotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya,
jambo linaloendelea kuhatarisha maisha ya watu, mali na maiundo mbinu inayojengwa
kwa gharama kubwa. Matumizi ya dawa haramu za kulevya ni chanzo kikuu cha vifo miongoni
mwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64. Ni chanzo kikuu cha ongezeko la mauaji
na vitendo vya jinai. Madhara ya matumizi haram ya dawa za kulevya yanaweza kupunguzwa
kwa njia ya elimu makini, kuzuia na kuponya kama mwelekeo sahihi katika kupambana
na matumizi haram ya dawa za kulevya.
Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inasema
matumizi haramu ya dawa za kulevya yanauletea mwili na afya ya binadamu hasara kubwa.
Matumizi yake ni kosa kubwa, isipokuwa kwa misingi tu ya tiba. Utengenezaji wa holela
na usafisrishaji wa dawa za kulevya ni mazoezi mabaya. Yanayounda ushirika wa uovu,
kwa kuwahimiza watu kuingia katika mazoea yaliyo kinyume kabisa cha sheria ya maadili.
Kumbe, kuruhusu matumizi ya dawa za kulevya ni jambo ambalo ni hatari na wala halina
mvuto! (Rejea, KKK no 2291).
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.