Jumuiya ya Kimataifa inahitaji mikakati ya kilimo makini na endelevu
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon pamoja na Bwana Josè Graziano da
Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, wanaitaka
Jumuiya ya Kimataifa kuibua sera na mikakati bora ya kilimo kama sehemu ya kushiriki
kikamilifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Familia ya Wakulima Kimataifa.
Ni wajibu
wa Serikali kusaidia mikakati ya wakulima wadogo wadogo kuweza kutekeleza wajibu wao
kikamilifu. Serikali ziwajengee uwezo familia za wakulima hasa vijana na wanawake,
kwa kuibua sera na mikakati itakayosaidia kukuza na kudumisha maendeleo ya sekta ya
kilimo vijijini.
Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na maboresho ya miundo
mbinu ya barabara, ili kupunguza kiwango cha uharibifu wa mazao unaofanyika tangu
mazao yanapovunwa mashambani hadi pale yanapomfikia mlaji. Benki na vyama vya kutoa
mikopo viwasaidie wakulima wadogo wadogo kupata mikopo ili kuinua kiwango cha uzalishaji.
Bwana
Graziano da Silva anasema kwamba, wakulima wadogo wadogo wakiwezeshwa katika uzalishaji,
Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa siku za usoni.
Utafiti uliofanywa katika nchi 93 unaonesha kwamba, asilimia 90% ya mashamba yanamilikiwa
na familia, ambazo pia ni wamiliki wa ardhi. Asilimia 63% ya mashamba Barani Ulaya
ndiyo yanayomilikiwa na familia.
FAO inasema kumezuka wimbi la kuwaponya wakulima
vijijini ardhi waliyokuwa wanaimiliki kwa kisingizio cha kutaka kuwekeza katika kilimo
cha kisasa, hali ambayo inaweza kusababisha kutoweka kwa amani na utulivu. Sheria
na kanuni za utawala bora na kanuni za uwajibikaji makini katika uwekezaji kwenye
sekta ya kilimo zinapaswa kuzingatiwa. Wawekezaji wataendelea kukwapua maeneo makubwa
ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kisasa, kumbe jambo la msingi inasema
FAO ni kuhakikisha kwamba, sheria na kanuni zinazingatiwa kwa ajili ya mafao ya wengi.