2014-03-20 11:43:21

Umuhimu wa vyama vya kitume katika maisha na utume wa Kanisa


Waamini walei nchini Angola na Sao Tomè wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa shupavu na wajasiri katika kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo adili, yenye mashiko na mguso kwa wale wanaowazunguka. Huu ni mwaliko uliotolewa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Angola na Sao Tomè katika mkutano wake wa mwanzo wa Mwaka uliohitimishwa hivi karibuni, huko Sao Tomè.

Tamko la Maaskofu Katoliki Angola na Sao Tomè lililotiwa mkwaju na Askofu mkuu Gabrieli Mbilingi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola na Sao Tomè anakazia umuhimu wa vyama vya kitume kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Vyama vya kitume vinapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, waamini walei wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kushirikiana na Makleri pamoja na Watawa.

Vyama vya kitume, vijenge na kudumisha utamaduni wa kushika sheria, kanuni na miongoz inyotolewa na Maaskofu mahalia, ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo, mshikamano na ustawi wa Kanisa la Kristo kuanzia ndani ya Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vigango, Parokia, Jimbo na Kanisa katika ujumla wake. Ikiwa kama vyama vya kitume vitashindwa kufuata sheria na kanuni, Kanisa linaweza kujikuta likiogelea katika kinzani zisizokuwa na msingi.







All the contents on this site are copyrighted ©.