Ulimwengu wa digitali unapaswa kuinjilishwa kwa njia ya imani tendaji!
Monsinyo Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anabainisha
kwamba, mabadiliko makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya
jamii ni changamoto kwa watu kubadili njia na mfumo wa mawasiliano unaojikita zaidi
katika majadiliano.
Huu ndio
mwelekeo unaotakiwa na vijana wa kizazi kipya wanaoendelea kuogelea katika ulimwengu
wa digitali, tofauti na Makleri waliozoea utamaduni wa kuzungumza na kusikilizwa pengine
hata bila ya kuulizwa maswali.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari
yanawezesha mchakato wa mawasiliano kuwa wa njia mbili: Hili ni jukwaa ambalo watau
wanajadiliana, wanashirikishana, wanaweza kuelewana au kusigana. Ni mahali pa kuchangia
hoja, hapa watu wanauliza maswali msingi ili kupatiwa majibu muafaka yatakayoweza
kukidhi hamu ya mioyo yao! Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
ya teknolojia ya habari mambo makuu matatu yanajenga msingi wa mawasiliano: Kusikiliza,
Kushirikisha na Kutia moyo!
Haya ndiyo mambo makuu ambayo yamelisukuma Kanisa
kujikita katika matumizi ya njia mpya za mawasiliano ya kijamii, kama inavyojionesha
kwa namna ya pekee kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anatumia mitandao ya kijamii
na kwamba, idadi ya wale wafuasi wake hadi sasa ni zaidi ya million kumi.
Hata
katika Injili, Yesu aliweza kuzungumza mambo makubwa kwa kutumia maneno macheche tu!
Kwa mfano Kheri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kama ilivyo pia
kwa Sala ya Baba Yetu wa Mbinguni. Huu ni mwaliko na changamoto kwa Maaskofu pamoja
na viongozi wengine wa Kanisa kuangalia jinsi wanavyoweza kutumia maendeleo ya sayansi
na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na Kweli za
Kiinjili.
Mitandao ya kijamii ni jukwaa lenye mazuri na mapungufu yake. Hata
Baba Mtakatifu Francisko alipoanza kutumia mitanao hii alikumbana na upinzani hata
wakati mwinginie na maneno ya kashfa na kejeri, lakini ni mambo ambayo hayakumkatisha
tamaa! Kuna baadhi ya watu walitaka kuhakikisha kwamba, anafunga akaunti yake mara
moja, lakini kwa bahati mbaya hawakufua dafu!
Baba Mtakatifu Francisko ameendelea
kutumia mitandao ya kijamii kadiri ya uwezo wake bila woga wala makunyanzi. Katika
mtandao wa Baba Mtakatifu @Pontififex, anatuma ujumbe, lakini si mara zote anawajibu.
Makanaisa mahalia wanaweza pia kujenga na kuendeleza jukwaa hili kwa kutumia kanuni
ya auni.
Matumizi ya mitandao ya kijamii yanayofanywa na Baba Mtakatifu yanaonesha
mafanikio makubwa kwa mfano wakati alipowaalika waamini kujiunga naye kusali kwa ajili
ya kuombea amani nchini Syria, kulikuwa na mwitiko mkubwa, licha ya ukweli kwamba,
Kanisa pia lilitumia njia za kawaida za mawasiliano ya Jamii ili kufikisha Ujumbe
wa Baba Mtakatifu kwa watu wengi zaidi. Katika kipindi cha muda mfupi tu, waamini
kutoka katika Majimbo, Parokia za Jumuiya zao walijikusanya na kuanza kuwashirikisha
wengine ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.
Monsinyo Paul Tighe anasema,
Vatican inaendelea kuboresha mfumo wake wa kupasha habari kwa kusoma alama za nyakati.
Leo hii kuna ushirikiano mkubwa kati ya vyombo na taasi za habari za Vatican kama
vile: Kituo cha Televisheni cha Vatican, Radio Vatican, Gazeti la L’Osservatore Romano;
vyombo vyote hivi vinapatikana kwenye mtandao wa habari ujulikanao kama News.va. Kwa
maneno machache maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yanawawezesha watumiaji
kutembea na Baba Mtakatifu mifukoni mwao!
Maendeleo yote haya ni fursa kwa
vijana kujieleza, kujifunza, kuhabarishana sanjari na ujenzi wa urafiki. Hadi sasa
wataalam wa mawasiliano ya kijamii hawana uhakika wa dira na mwelekeo wa njia hizi
za mawasiliano kwa siku za usoni, kwani s itu kwamba zinaleta mabadiliko, bali pia
watumiaji wa mitandao hii wanabadilisha namna yao ya kufikiri na kutenda, ikilinganishwa
na miaka kadhaa iliyopita. Kuna mabadiliko makubwa ya jinsi ya kujenga na kuimarisha
Jumuiya za waamini wanaojisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa linalopaswa kushuhudia imani
yake.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita alishawahi kudokeza
kwamba, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina na kuangalia taalilimungu inayobebwa
kwenye mitandao ya kijamii, ili kuweza kuitumia kikamilifu! Waamini wajifunze lugha
ya utamaduni mpya wa digitali, ili kuweza kumwilisha Injili ya Kristo katika jukwaa
hili jipya la mawasiliano ya Jamii. Waamini wawe makini kuchagua yale yanayofaa katika
maisha na utume wao kama Wakristo na kuangalia mambo ambayo pia yanapaswa kubadilishwa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa haliwezi kuwa mtazamaji katika matumizi
ya mitandao ya kijamii, bali linapaswa kuingia na kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa kuitakatifuza mitandao hii kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Jukwaa hili linawakusanya
mamillioni ya watu wanaotumia muda mrefu kupata na kutoa habari.
Kanisa lisipojiingiza
kikamilifu katika Jukwaa la mitandao ya kijamii, litashindwa kuwafikia waamini katika
uhalisia wa maisha yao! Hii ni hija ya ambayo inapania kumwezesha mwamini kukutana
na kuzungumza na Yesu; kwa kujali na uvumilivu mkubwa; kuwajibika na katika ukweli;
kwa kuzama katika tamaduni na lugha za mitandao ya kijamii bila kusahau kubeba ”mtumba
wa imani tendaji”.
Meandaliwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.