Serikali ya Pwani ya Pembe inaendelea kufanya sensa ya watu na makazi, zoezi ambalo
linafanyika nchini humo baada ya kuyoyoma miaka kumi na sita. Viongozi wakuu wa Serikali
ya Pwani ya Pembe ndio waliofungua mchakato wa sensa ya watu na makazi. Serikali inatarajia
kutumia kiasi cha Euro millioni 18 hadi kukamilika kwa zoezi zima ambalo linatarajiwa
kufanyika katika kipindi cha mwezi mmoja.
Sensa ya watu na makazi iliyofanyika
kunako Mwaka 1998 ilionesha kwamba, Pwani ya Pembe ilikuwa na watu millioni 16. 3.
Kunako Mwaka 2008, Pwani ya Pembe haikufanikiwa kufanya sensa ya watu na makazi kutokana
na machafuko ya hali ya kisiasa nchini humo yaliyodumu kwa takribani miaka minane.
Kwa sasa inakadiriwa kwamba, Pwani ya Pembe ina jumla ya wananchi millioni 24, lakini
usahihi wa takwimu hizi utathibitishwa na Sensa ya Watu na Makazi inayoendelea nchini
humo.