2014-03-20 11:26:03

Hali ya kisiasa ni tete nchini Burundi


Serikali ya Burundi imekipiga rufuku Chama cha upinzani cha Mshikamano na Maendeleo, Msd, kwa kipindi cha miezi minne kutokana na kusababisha fujo na vurugu mjini Bujumbura hivi karibuni. Hayo yamebainishwa na Waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Edouard Nduwimana. Homa ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Burundi kunako mwaka 2015 inazidi kupamba moto, jambo ambalo linaendelea kusababisha hofu na wasi wasi wa kutoweka kwa misingi ya haki, amani na utulivu.

Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka Bwana Francois Nyamoya, Katibu mkuu wa Chama cha Mshikamano na Maendeleo nchini Burundi ambaye anasema kwamba, kitendo hiki ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu, lakini anawataka watu wanaomuunga mkono kuheshimu maamuzi ya Mahakama, ili kulinda amani na utulivu nchini Burundi.

Jeshi la Polisi pia linawasaka kwa udi na uvumba wanachama wengine wa Msd kwa kusababisha vurugu na ikiwa kama watapatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa kufungwa jela maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.