2014-03-19 11:18:16

Wakimbizi, Sudan ya Kusini wanakabiliwa na hali ngumu!


Umoja wa Mataifa unasema hali ya wakimbizi Kusini mwa Sudan inatisha kwani hadi sasa kuna zaidi ya wakimbizi 77, 000 wanaopewa hifadhi kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Malakal na kwamba, bado kuna hali ya wasi wasi kuhusu vita inayoendelea Sudan ya Kusini. Hili ni kundi la raia ambalo limelazimika kuyakimbia makazi yake kutokana na machafuko ya kisiasa nchini humo, kumbe linahitaji kupatiwa msaada wa dharura.

Umoja wa Mataifa unafikiria kuanzisha kambi nyingine za wakimbizi ili kuboresha maisha ya wakimbizi hawa ambao kwa sasa wanaendelea kufurika siku hadi siku. Mvua zilizoanza kunyeesha zinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, ikiwa kama hatua za dharura hazitachukuliwa mapema iwezekanavyo. Hadi sasa wadau wakuu katika vita inayoendelea Sudan ya Kusini hawajaridhia uwepo wa Jeshi la kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika ambalo lilipaswa kuwasili nchini humo, kati kati ya Mwezi Aprili, 2014.

Huu ulikuwa ni uamuzi uliotolewa na IGAD kama sehemu ya mchakato wa kusitisha vita Sudan ya Kusini, katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni, huko Addis Ababa, Ethiopia. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika kinalenga kudumisha amani na usalama kwa raia na mali zao pamoja na kuhakikisha usalama kwenye visima vya mafuta, Sudan ya Kusini.







All the contents on this site are copyrighted ©.