2014-03-18 10:05:39

Punguzeni mishahara yenu, ili kugharimia maendeleo ya wananchi wa Kenya!


Askofu mstaafu Alfred Rotich wa Jimbo la Kijeshi Kenya, amewataka wananchi wa Kenya kutambua kwamba, wanahitaji viongozi waaminifu, wakweli na wazalendo, wanaoweza kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, viongozi wanaoguswa na shida pamoja na mateso ya wananchi wao.

Jamii inahitaji viongozi mahiri watakatoa dira na mwelekeo wa maisha badala ya kuwa na viongozi wanagubikwa na uchu wa mali na madaraka, viongozi wanaojitafuta wenyewe. Viongozi na watumishi wa Serikali waguswe na mahangaiko ya wananchi wa kawaida, ili waweze kupunguza mishahara minono wanayopokea kwa kutambua kwamba, huu ni mchango na sadaka kubwa inayofanywa na wananchi wa kawaida kabisa.

Kitendo cha Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake kupunguza kiwango cha mishahara yao kwa asilimia 20% ni jambo linalotia moyo na linapaswa kuigwa na wafanyakazi wengine wa Serikali na Umma. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa umepelekea watu wengi kukosa fursa za ajira. Majadiliano kuhusu upunguzaji wa kiwango cha mishahara yanaendelea kuungwa mkono na Makatibu wakuu wa Wizara ambao wameamua kukwata asilimia 10% ya mishahara yao.

Mazungumzo haya yaendelezwe kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali, lengo likiwa ni kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi wa Kenya. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 55% ya Kodi yote inayokusanywa inatumika kulipia mishahara. Hii ni sawa na asilimi 13% ya Pato Ghafi la Taifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.