Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2013 alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki,
kwa unyenyekevu na moyo mkuu akaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, huku
akizungukwa na bahari ya sala na sadaka iliyokuwa inatolewa na watu mbali mbali ndani
ya Kanisa.
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mchumba wake
Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 19 Machi
2013 akaanza rasmi kuliongoza Kanisa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa
wa viongozi wa Kanisa, Serikali na Dini mbali mbali.
Baba Mtakatifu Francisko
katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, anapenda kutoa shukrani zake
za dhati kwa wote wanaomkumbuka kwa sala na matashi mema wakati huu anapoadhimisha
Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Anawasihi kuendelea kusali
kwa ajili yake na Kanisa kwa ujumla.