2014-03-17 12:11:56

Watanzania wanamkumbuka Marehemu Padre Egidio Guidi


Ndugu Egidio Guidi alizaliwa katika Parokia ya Premilcuore – Jimbo la Forli, Provinsi ya Toscana, mnamo tarehe 17 Machi 1933. Akiwa na miaka mitatu alifiwa na mama yake na kulelewa na Edvige Mussolini, Dada wa aliyekuwa Benito Mussolini, (Fashisti) na mtawala wa nchi ya Italia wakati wa vita ya pili ya dunia. Angali bado mdogo na akiwa na miaka 12, alijiunga na seminari ndogo.

Mwaka 1950, baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari na akiwa na umri wa miaka 17 tu alijiunga na ndugu Wakapuchini katika Provinsi ya Toscana kwa kuanza malezi ya Novisiati. Mwaka moja baadaye Septemba 8, 1951, alisherekea nadhiri zake za kwanza. Miaka mitatu baadaye Septemba 12, 1954 alifunga nadhiri zake za daima. Akiwa na miaka 25, Machi 22, 1958 Ndugu Egidio alipewa daraja la Upadre.

Umisionari: Kutokana na hamu yake ya kuwa Mmisionari katika nchi za Afrika, aliomba kwa wakubwa wake kuja katika nchi ya Tanganyika (Tanzania) na ombi lake lilikubaliwa. Tarehe 2, Juni 1963 akiwa na wenzake wanne, akiwa na umri mdogo kuliko wenzake, walikabidhiwa, msalaba wa Umisionari, na ndipo tarehe 6 Juni, 1963, kwa kutumia meli, walianza, safari ya kuja katika nchi ya Tanganyika (Tanzania). Baada ya meli yao kutua nanga katika bandari ya Dar es salaam alielekea Pugu, ambapo kwa muda alikaa katika parokia hiyo.

Mwezi Julai, 1963 pamoja na wenzake walianza safari kuelekea Dodoma kupitia Iringa ambapo tarehe 28 Julai 1963 walienda sehemu ya Kondoa kwenye Parokia ya Haubi na Itololo kwa ajili ya kujifunza lugha ya Kiswahili.

Utume na Sehemu alizoishi kufanya kazi: Mnamo Desemba 8, 1963 alielekea katika Parokia ya Mpwapwa. Katika utume wake kwenye Parokia ya Mpwapwa kama Paroko msaidizi, Utume wake ulihusisha kazi za kiofisi, shule za msingi, sekondari na Chuo cha Ualimu. Kwa usafiri wa lori aliloendesha mwenyewe aliweza kuzunguka eneo kubwa la vigango vya Kongwa hadi Mlali (wakati huo). Ilichukua muda kwa baadhi ya Wakristu kufahamu kama ni Padre kwani walifikiri ni dereva tu wa lori mpaka walipomwona tena altareni kwenye adhimisho la MisaTakatifu.

Akiwa bado katika Parokia ya Mpwapwa aliweza pia kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mapadre, Masista, kiwanda cha kupasua mbao, makanisa ya Vigango vya Kisokwe, Godegode na Tubugwe, na pia kuanzisha jengo la chekechea. Changamoto iliyotokana na Uhuru wa Tanganyika (1961) ilikuwa baada ya uhuru baadhi ya watu hawakuweza kutofautisha Wamisionari na Wakoloni.

Wakati mwingine watu hawakuweza kuwasaidia au kuwasikiliza wakifikiri ni Wakoloni waliosalia. Baadaye watu waliendelea kuwazoea na kuwapokea na kuwaona kweli wao ni Wamisionari na sio wakoloni waliosalia.

Kutokana na hitaji katika Parokia ya Kongwa, mnamo Oktoba 10,1968, alihamia Kongwa sehemu ya Morisheni, walipokaa Washeli- sheli kutoka Mauritania. Akiwa Paroko Msaidizi wa Kongwa, mwaka 1971, alitumwa kwenda Kigango cha Mlali ili kujenga Kanisa, nyumba ya Mapadre, nyumba ya Masista, shule ya chekechea – kusudi Mlali iwe Parokia baadaye. Ujenzi huo ulikamilika mwaka 1975, kisha Askofu Mathias Isuja alipofika kubariki Jengo, alitangaza Mlali kuwa Parokia. Ndugu Egidio akabaki Mlali na kuwa Paroko msaidizi.

Hatimaye Januari 20, 1977 alipata uhamisho kwenda Parokia ya Mbuga na kuwa Paroko, baada ya kukosekana mtu wa kumtuma Mbuga. Ndugu Egidio alijitolea. Mbuga ilihudumiwa na Mapadri Wapasionisti tangu mwaka 1940 hadi mwaka 1958 ilipotangazwa kuwa Parokia. Ndugu Egidio, alikaa kwa miaka 24 na miezi 11 Mbuga akiwa kama Paroko. Kama paroko hakubaki tu ofisini kuwasuburi waumini, ila alikuwa pia dereva, na fundi wa mambo mbalimbali, na pia aliweza kutoa huduma za Kiroho na kusimamia ujenzi wa vigango vipya vya Uleling`ombe, Galigali, Matonya, Mandasi, Mtamba na Kizi.

Kwa vile hapakuwa na hospitali eneo hilo, alilazimika kuwapeleka wagonjwa umbali wa Kilometa 84 kwenye hospitali ya Mpwapwa kwa nyakati zote hasa usiku, na pale wenyeji walimwita jina“ Chausiku” kwani wakati mwingine ilibidi kusafiri usiku kumfikisha mgonjwa hospitali, au kurudi usiku kwenye kituo chake cha Parokia ili Waumini wasije wakakosa huduma za kiroho. Akiwa katika Parokia hiyo aliweza kuwapeleka vijana wengi kwenye miito mbalimbali, kwa upande wa mapadre wapo mapadre 13 na kwa upande wa Masista hata yeye hajui ni wangapi amewapeleka Utawani.

Mnamo Julai 2002 aliteremka tena toka Parokia ya Mbuga hadi Parokia ya Kongwa ambapo alikuwa Paroko msaidizi hapo. Hapo ndipo Mhudumu wa Provinsia alipomwomba kuwa karibu na kuratibu masuala ya ujenzi wa Kanisa la Mkoka. Mei 24, 2005 kwa maridhiano ya Mhashamu Askofu Mathias Isuja – aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma na kibali kutoka kwa Mhudumu wa Provinsia aliwekwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mkoka.

Lengo lilikuwa kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mapadre na Jengo la Kanisa. Hata hivyo Egidio hakuishia hapo, kwani alianzisha ujenzi wa shule ya awali ya Nazareti, nyumba ya masista, stoo, jiko, mradi wa mashine ya kukamua alizeti kwa lengo la kusaidia jamii na kutegemeza Parokia.

Toka wakati huo pia aliendelea na ujenzi na ukarabati wa makanisa katika vigango vya Chitego, Norini, Banyibanyi, Silale, Leganga, Chigwingwili, Songambele, Matongoro na Makawa.

Kila mahali ambapo Mwenyezi Mungu amemjalia kukaa katika utume wake: yaani Mpwapwa, Kongwa, Mlali, Mbuga na Mkoka aliwahudumia Taifa la Mungu na Jamii Kiroho na Kimwili (hasa wakati wa njaa). Pia amebahatika kupokea watoto wachanga kwa ruhusa ya pekee ya Askofu Mathias Isuja na kuishi nao misioni, kuwasomesha na kuwapatia mahitaji ya msingi kwa maisha yao hadi kifo chake.

Lakini sio wao tu bali hata watoto wa wasaidizi wake wa karibu katika kazi mbalimbali waliofariki na kuacha watoto wadogo amelazimika kwa kuthamini majitoleo ya wazazi wao kuwatunza kwa kuwasomesha watoto hao wapatao zaidi ya 40 kwa misaada ya Wafadhili. Anaeleza kwamba maisha ya watoto wa namna hii yananigusa sana kwani hata yeye ni mtoto yatima ambaye alilelewa na Masista na Mapadre mpaka amekuwa Kasisi na Mmisionari.

Mungu amemwita katika makao yake ya milele akiwa na miaka 81 ya kuzaliwa, 64 ya Utawa, 56 ya Upadre na 51 ya Umisionari. Ndugu Egidio alipenda sana kusimulia hadithi mbalimbali, na matukio mbalimbali ya maisha. Alikuwa msimulizi wa kuvutia na asiyechoka na bila kuchosha. Pia, alikuwa mtu asiyepitwa na wakati, alijiendeleza kwa kusoma na kutafuta habari mbalimbali za kidunia.

Lakini, zaidi ya yote ndugu Egidio alikuwa mwenye moyo mkubwa, mwenye kujaa utu, mkarimu, mpenda watu, mwenye huruma kwa waliohitaji. Mtu wa sala na ibada kubwa. Ni mtu aliyemtegemea Mungu kwa karibu kila kitu. Hata siku anapelekwa hospitali, njiani alishauri gari isimamishwe na kumwomba Padre mwenzake ampe huduma ya maungamo na mpako wa wagonjwa. Ni kama alijua kifo chake kinakuja, kwa furaha aliwasalimia watu na kuagana kuwa hasa wajitahidi katika kazi zao.

Alijitambulisha na kujifananisha na watu aliofanya nao kazi. Hata siku za mwisho hakuona sababu tena ya kwenda likizo. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Maisha yake na kumwombea Mungu ampokee kwenye uzima wa milele. Raha ya Milele UmpeEe Bwana na Mwanga wa Milele Umwangazie – Apumzike kwa Amani – Amina.








All the contents on this site are copyrighted ©.