2014-03-17 09:02:08

Usawa wa kijinsia katika Bunge Maalum la Katiba Tanzania wapongezwa


Mtandao wa Wanawake na Katiba wenye mashirika zaidi ya 50 yanayotetea haki za wanawake katika Katiba mpya, umepokea kwa furaha mchakato na matokeo ya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa Bunge Maalum la Katiba (Mwenyekiti na Makamu wake) ambao umezingatia usawa wa jinsia.

Pamoja na kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Mwaka 2012 haikuanisha kuwa uchaguzi wa uongozi wa Bunge hili uzingatie usawa wa jinsia, tumetambua busara na hekima za wajumbe za kuonyesha nia ya kujenga msingi wa usawa wa jinsia katika uongozi na vyombo vya maamuzi nchini. Kwetu sisi, hili si suala la uwepo wa mwanamume na mwanamke katika uenyeketi wa Bunge Maalumu tu, bali pia ni ukomavu wa kipekee wa wajumbe katika kuuona ukweli kuwa suala la kuimarisha sauti za wanawake na wanaume ni nyeti sana, haswa wakati wa ujenzi wa maridhiano muhimu kikatiba.

Tunawapongeza waliochaguliwa ambao ni Mhe. Samweli Sitta (Mwenyekiti) na Mhe. Samia Hassan Suluhu (Makamu Mwenyekiti) kwa kuaminiwa katika nyadhifa hizo muhimu. Mtandao wa Wanawake na Katiba unatambua uwezo wao katika utendaji na una matumaini makubwa kuwa pamoja na mengine mengi watakayoyasimamia, watatoa uongozi ulio imara na wenye weledi wakati wakiongoza Bunge hili katika kujadili na kupitisha misingi muhimu itakoyopelekea katika ujenzi wa usawa wa kijinsia nchini.

Tunategemea kuona usawa wa jinsia ndani ya Katiba mpya, ambao sio ule tu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali, lakini pia usawa ulio na nia ya kujenga misingi ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi walio wengi na haswa wanawake nchini.

Kwa mtazamo huu, tunatarajia kuwa busara za Wenyeviti hawa na washauri wao zitatumika pia kuzingatia usawa wa kijinsia katika Kamati zitakozoundwa pamoja na kuwa kuzingatia ustadi na uzoefu wa wanakamati unahitajika. Nia kubwa ikiwa kuona wanawake kwa wanaume watatoa sauti zao kuhakikisha na kulinda, pamoja na mengine, uzingatiwaji wa usawa wa jjinsia katika vifungu vyote vya Katiba mpya.

Vilivile, Mtandao wa Wanawake na Katiba, unawapongeza wajumbe wote wanawake kwa umoja wao, mshikamano na ushirikiano imara, ambao umeleta mafanikio makubwa katika michakato inayoendelea huko Dodoma kwenye Bunge Maalumu. Huu ni mwanzo wenye kuonyesha mifano mizuri, na ambao tunapenda kuuona ukiendelezwa na kusimamiwa imara wakati wote Bunge Maalumu litakapokuwa likifanya kazi yake ya kuchambua na kupitisha vifungu mbalimbali vya Katiba,








All the contents on this site are copyrighted ©.