2014-03-17 08:27:47

Tafadhali sana! Msikomae katika uchoyo na ubinafsi!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani. RealAudioMP3

Katika kipindi cha Kwaresma tunatafakari na tunakiri udhaifu wetu na tunajibidisha kukomesha vilema vyetu vya roho na mwili ili tumpendeze Mungu na tuwe watu wanaofaa katika familia na katika jamii ya wanadamu. Dhamira ya jumla inayotubeba katika kipindi hiki cha Kwaresma ni wito wa kumrudia Mungu, kurudi katika njia za haki, ili tustahili kukaa katika hema yake takatifu.

Bwana anatualika kipindi hiki, kusali, kutoa sadaka na kufunga. Katika kipindi kilichopita tulitazama kwa ufupi juu ya tunu ya sala. Leo tutafakari juu ya tunu ya kutoa sadaka. Sadaka ni nini? Kwa tafanusi nyepesi, sadaka ni neno, hali au kitu ambacho mtu hutoa kwa mtu kwa ajili ya mafaa ya mwingine kiroho au ya kimwili. Hivyo kuna sadaka za maneno (ushauri mwema), sadaka za vitu, kuna sadaka za hali na kuna sadaka za sala pia. Tangu zamani za wazee wetu, mfungo wowote ule uliambatana na sadaka. Watu walimtolea Mungu sehemu ya mali zao kama alama ya shukurani au alama ya kuomba baraka na huruma ya Mungu.

Sisi nasi katika mfungo wetu wa Kwaresma tunahimizwa kutoa sadaka zaidi, kwa ajili ya kulitegemeza Kanisa na kuwasaidia wanadamu wenzetu walio wahitaji katika haki. Wapo masikini ambao wanashindwa kabisa kuyamudu maisha yao ya kila siku kutokana na sababu mbalimbali halali. Hatuwezi kuwasukumizia hao pembezoni au hatuwezi kuziba macho kana kwamba hatuwaoni. Hao ni sehemu ya Kristo mteswa, aliyependa kujiweka ndani ya wahitaji kama vile wenye njaa, wagonjwa, walio uchi, wenye kiu, wafungwa na wageni. (Rej. Mt. 25:31…)Tunahimizwa kutoa sadaka ili kuwagusa watu kama hao. Kufanya hivyo, ni kumgusa yesu mteswa mwenyewe.

Lakini ikumbukwe kwamba, kutoa sadaka ni tendo la kimungu na ni tendo la kiibada. Ni tendo linalolenga kwanza kabisa kumpa Mungu heshima na pili kumsaidia mwanadamu mhitaji. Hivyo kutoa sadaka ni tendo takatifu, na kinachotolewa lazima kiwe na thamani machoni pa Bwana. Hapa kuna mambo mawili, yaani kitu kinachotolewa na namna kinavyotolewa. Haya mawili yakiunganishwa vizuri ndipo haswa mtoaji hutuzwa na Bwana.

Bwana mwenyewe katika neno lake anatupatia nidhamu ya kutoa sadaka anaposema “angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu ili mtazamwe na wao...(Mt. 6;1-6).
Neno hili, litusaidie kukwepa sana kishawishi cha nyakati zetu hizi, cha kupenda kujitukuza katika masikini na wahitaji. Sisi tunaomwamini Kristo, tuone na tuonje uwepo wa Kristo mteswa katika maskini na wahitaji. Bwana aonya, tukitoa sadaka kama wanafiki wafanyavyo, ili tutukuzwe na watu, hatutapata thawabu yoyote mbele ya baba wa mbinguni. Sadaka yetu iwe ni kwa siri, (sisi tunaongeza, iwe kwa siri na kwa heshima). Isiwe sadaka ya kudhalilisha utu wa mtu, au sadaka ya kumuanika mtu hadharani.

Nyakati zetu hizi zinashuhudia aina ya watu ambao, hawawezi kutoa sadaka kwa maskini, hadi TV zote ziwepo na waandishi wa habari wa magazeti yote wawepo. Huko ni kujitukuza!!. Bwana asema ‘...hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume’. Sasa unavyokaa unaanika yatima kwenye TV ili uonekane unatoa sadaka ya sabuni na chumvi, huoni kama unaisaliti Injili? Huoni kama unadhalilisha hao unaowaanika kwenye vyombo vya habari ili ujitukuze wewe kama mtoaji? Kuna namna nyingi za heshima za kuielimisha jamii juu ya kuwasaidia wahitaji, kuliko kuwinda nyakati fulani za kujionesha.

Tunaalikwa kutoa sadaka za neno jema pia, kushauri wenye mashaka ya maisha. Lakini nayo ifanyike kwa heshima na siri. Hatuwashauri watu halafu baadaye tunaanika mtaani yoote tuliyoshauri. Hapo tunaharibu usadaka ya sadaka yetu. Tusisahau kutoa sadaka ya sala, kuliombea Kanisa na watu wote ulimwenguni. Sadaka ya sala yenye nia njema haipotei kamwe.

Mpendwa msikilizaji, tunaendelea kuliangukia Kanisa la nyumbani ambalo ni shule ya upendo! Wazazi tusisahau kuwafundisha watoto wetu roho ya ukarimu. Kupenda kutoa sadaka kuwasaidia wahitaji. Watoto wetu wazoeshwe kutoa sadaka kulitegemeza Kanisa. Watoto wetu wasikomae katika uchoyo na ubinafsi. Ni jukumu letu kupanda mbegu ya ukarimu ndani ya watoto wetu.

Na sisi sote kama familia, kwaresma hii, tuwe na sadaka ya pamoja. Tufungue macho kwa upendo tuwatazame wahitaji, tukunjue mikono kwa ukarimu tuwasaidie hao wahitaji. Ifike mahali tuone furaha katika kutoa sadaka, kwani tunafundishwa, “kupokea kunaijaza mikono bali kutoa huujaza moyo, na kupokea kwa shukurani kwampendeza Mungu”.
Wapendwa wanafamilia-Kanisa la nyumbani, TUTOE SADAKA, lakini ikwepwe kabisa tabia ya kutoa yale ambayo hatuyahitaji, yale ambayo hayana maana tena kwetu. Unatoa nguo zilizochakaa kabisa au unatoa sadaka ya nguo chafu kupindukia, au unatoa vyakula vilivyo haribika kabisa. Hapo hutoi sadaka bali unatoa takataka, yaani unasafisha nyumba yako. Masikini na wahitaji NI WATU, sio jalala la takataka. Toa kile ambacho hata wewe mwenyewe unakihitaji. Sadaka huwa inauma, lakini inaleta furaha rohoni ukiitoa kwa moyo. Tena katika kutoa sadaka ya kweli, TUNAWASAIDIA WANADAMU WOTE bila ubaguzi wala upendeleo.

Tujijengee moyo wa sadaka, ili kwa njia ya sala, sadaka na matendo yetu, sote tuwe wapendevu machoni pa Mungu wetu naye mwenyewe kwa msaada wa neema zake atusaidie tuwe sadaka yenye harufu nzuri machoni pake, na mwisho wa uzima huu sote tukastahili kukaa hemani mwa Bwana. Bwana awabariki na kuwatuza wote wanaotoa kwa ukarimu.
Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.