2014-03-17 11:29:01

Papa Francisko kuongoza kesha la sala dhidi ya vitendo vya Mafia nchini Italia


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 21 Machi 2014 anatarajiwa kukutana na Chama cha Libera kilichoanzishwa na Don Luigi Ciotti kama sehemu ya mchakato wa kupambana na kikundi cha kigaidi cha Mafia nchini Italia ili kukuza na kudumisha utamaduni wa utawala wa sheria. Chama hiki kinashirikisha vyama vipatavyo 1,500, ili kupambana na Kikundi cha Mafia. Baba Mtakatifu atakutana na wanachama wa Chama hiki kwenye Parokia ya Mtakatifu Gregori VII, iliyoko kwenye eneo la Vatican.

Katika tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza kesha la sala kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na jamaa wa watu ambao wameathirika kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Mafia nchini Italia. Kilele cha maadhimisho ya siku ya kumi na tisa, itakuwa ni hapo tarehe 22 Machi 2014 mjini Latina.

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 7,000 wanaowawakilisha watu 11, 000 nchini Italia wamepoteza ndugu, jamaa na rafiki zao kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Mafia. Ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko ni zawadi na faraja kubwa kwa watu ambao wamepoteza ndugu zao kutokana na vitendo vya kigaidi na kwamba, Baba Mtakatifu anajali na kuguswa na mateso ya watu hawa.







All the contents on this site are copyrighted ©.