2014-03-17 09:55:33

Changamoto zinazoikabili Sekta ya Maji Tanzania


Serikali ya Tanzania inaadhimisha Juma la Maji kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 22 Machi. Lengo ni kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kubainisha mikakati inayopewa kipaumbele ili kukabiliana na changamoto za huduma ya maji nchini Tanzania. Ni fursa kwa wadau mbali mbali wa maji kuweza kubadilishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo. Maadhimisho ya Maji Kitaifa kwa Mwaka 2014 yanafanyika Mkoani Dodoma kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Maji na Nishati”

Serikali ya Tanzania imesema ipo changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji nchini hali inayosababisha upatikanaji wa maji kuwa wa taabu. Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Mkoani hapa.

Alisema mbali na mabadiliko ya tabia nchi, uharibufu huo unasababishwa
na ongezeko la watu pamoja na shughuli za kibinadamu wanazozifanya
katika vyanzo hivyo vya maji "Ukitaka kujua tatizo la upungufu wa maji ni kuangalia miaka 15 liyopita ambapo kila mtanzania alikuwa akitumia meta za ujazo 2500kwa mwaka lakini kwa sasa imepungua na itakapofika mwaka 2020 kila mtanzania atatumia meta za ujazo 1700 tu," alisema.


Profesa Maghembe alisema hali hiyo inaonyesha jinsi ambavyo
upatikanaji wa maji unavyozidi kupungua mwaka hadi mwaka alibainisha kwamba changamoto ni kubwa na zinahitaji uelewa wa wananchi katika shughuli zao za kimaendeleo na kuchukua hatua ili kuhakikisha maji yanaendelea kuwepo. Kuhusu miundombinu alisema kumekuwepo na tatizo la watu kuifuata miundombinu ya maji kwamba sheria za adhabu zilizopo ni ndogo hivyo wanajipanga kupeleka mabadiliko katika sheria hiyo ili kuwa na kifungo kukomesha tabia hiyo.

Akizungumzia kuhusu miradi ya maji, Profesa Maghembe alisema zaidi ya
miradi 1600 ya maji inatekelezwa vijijini katika wilaya zote nchini
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14. "katika miradi hiyo mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Februari 2014, zaidi ya watu milioni 17 wanapata majisafi na salama "Ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015 tunatarajia idadi ya upatikanaji wa maji iongezeke kutoka watu asilimia 51.09 kufikia asilimia 74 nchini kote kwa idadi ya wanaoishi vijijini ambao ni asilimia 77," alisema Waziri huyo.

Aidha, alisema pia kwamba Serikali inapania kufikisha katika miji mikuu yote huduma ya majisafi kwa asilimia 85 katika kipindi cha Mwaka 2014. Upande wa Mkoa wa Dodoma, alisema miradi 69 katika vijiji 64 itakelezwa na itakapokamilika itakuwa imeinua kiwango cha upatikanaji wa maji.








All the contents on this site are copyrighted ©.