2014-03-15 09:39:06

Vitendo vya kigaidi nchini Nigeria vinachochewa na rushwa na ufisadi wa mali ya umma


Viongozi wa Makanisa nchini Nigeria wanalaani vikali tabia ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kuwatesa wananchi wa Nigeria nyakati hizi. Hayo yamesemwa na Kardinali John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Kanisa kuu la Kumbu kumbu ya Askofu mkuu Vinning wa Kanisa Anglikana lilipozinduliwa.

Kardinali Onaiyekani anasema kwamba, katika safari zake ndani na nje ya Nigeria watu wengi wanaendelea kumuulizia inakuaje, Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kinaendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia nchini Nigeria? Ushauri ambao anapenda kumpatia Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ni kuhakikisha kwamba, anakula sahani moja na Mafisadi wanaoiba fedha na utajiri wa Nigeria kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Hii ndiyo fedha chafu inayotumika kugharimia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. Fedha na utajiri unaotumika kununulia silaha dhidi ya raia, kama ungetumika kwa hekima na busara ungeweza kuchangia katika kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi wa Nigeria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linatarajia kwa siku za hivi karibuni kukutana na kuzungumzia kuhusu hali tete inayoendelea kujitokeza nchini Nigeria kiasi cha kusababisha hofu na wasi wasi.

Askofu James Odedeji wa Kanisa Anglikani wa Jimbo la West, Nigeria anasema, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ni vitendo vya kinyama, vinavyoendelezwa na rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na baadhi ya wanasiasa nchini Nigeria. Serikali haina budi kutekeleza dhamana yake ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.

Tangu mwaka 2009 hadi wakati huu, zaidi ya Wakatoliki 5,000 wameuwawa kikatili, Makanisa 20 na nyumba kadhaa kuchomwa moto na Kikosi cha Kigaidi cha Boko Haram ambacho kwa sasa kimekuwa ni tishio kwa maisha na mali ya wananchi wa Nigeria. Haya ni mashambulizi yanayofanywa kwa misingi ya kidini na rushwa inayoendekezwa na baadhi ya wanasiasa. Inasikitisha kuona kwamba, kuna kikundi kidogo cha watu ambao wanakalia utajiri mkubwa wa Nigeria kwa ajili ya mafao ya binafsi, wakati mamillioni ya watu wanaendelea kuteseka kwa vita, njaa, umaskini na maradhi.

Mwanzoni Kikundi hiki kilianzishwa na kufadhiliwa na baadhi ya wanasiasa waliokuwa wanataka kulinda na kutetea masilahi yao binafsi, lakini baadaye Kikundi hiki cha Boko Haram kimechukua mwelekeo mpya na kuwa ni Kikundi cha Kigaidi chenye mwelekeo pia wa kidini, ingawa hata Waamini wa dini ya Kiislam wanashambuliwa nacho pia.







All the contents on this site are copyrighted ©.