Professa Giuseppe Profiti kuendelea kuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesu, Roma
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa madaraka aliyokabidhiwa na Baba
Mtakatifu Francisko amemteua Professa Giuseppe Profiti kuendelea kuwa ni Rais wa Hospitali
ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican kwa kipindi cha miaka mitatu
yaani kuanzia Mwaka 2014 hadi Mwaka 2016. Kardinali Parolin ameteuwa pia Baraza Jipya
la Hospitali litakalofanya kazi zake kwa kipindi cha miaka mitatu pia.
Professa
Giuseppe Profiti mwenye umri wa miaka 52, tangu Mwaka 2008 amekuwa ni Rais wa Hospitali
ya Bambino Gesù. Katika kipindi cha uongozi wake, kumekuwepo na mafanikio makubwa
katika utoaji wa tiba kwa watoto wagonjwa, huduma za utafiri kiasi cha kuifanya Hospitali
hii kuwa ni Kituo kikuu cha utafiti wa magonjwa ya watoto Barani Ulaya. Hospitali
imepanua huduma zake kwa kuongeza matawi mengine nje ya Mji wa Roma.
Hospitali
ya Bambino Gesù imeendelea kuwa ni kielelezo cha huduma ya upendo na mshikamano kwa
watoto wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa kukosa huduma bora za tiba kama
vile: Cambodia, Yordan, Lebanon na Tanzania ambako imesaidia kujenga Kliniki ya Upasuaji
kwa watoto wenye ugonjwa wa moyo, kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Sindiga,
Tanzania.