Padre Guidi Egidio amefariki dunia, mazishi yatafanyika tarehe 18 Machi 2014, Jimboni
Dodoma
Mwanzilishi wa Parokia ya Mlali Jimbo Katoliki Dodoma Padre Guidi Egidio amefariki
dunia Ijumaa, tarehe 14 Machi, 2014 majira ya saa tisa na nusu alasiri katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Shirika la
Ndugu Wafransisco Wakapuchini Tanzania Padre Wolfgang Pisa imebainisha kuwa Padre
Egidi alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mapafu.
Padre Pisa amesema kuwa ibada
ya kumwombea Padre Egidi itafanyika katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mchumba wa
Bikira Maria Mkoka tarehe 17 Machi 2014 na kufuatiwa na mkesha Parokiani hapo. Amesema
kuwa mazishi ya Padre Egidi yatafanyika tarehe 18 mwezi huu katika makaburi ya Shirika
katika Parokia ya Kongwa saa tano kamili asubuhi.
Itakumbukwa kuwa Padre Egidi
hadi mauti yanamfika alikuwa Paroko wa Parokia ya Mkoka na vile vile alikuwa mkurugenzi
wa idara ya muziki Jimbo Katoliki Dodoma. Marehemu Padre Egidi alizaliwa tarehe 17.3.1933
nchini Italia na mara baada ya majiundo yake ya upadre alikwenda nchini Tanzania kunako
mwaka 1963.
Padre Egidi katika utume wake amefanya kazi za utume katika Parokia
za Kibakwe, Mpwapwa, Kongwa, Mlali na Mkoka. Padre Egidi amefariki akiwa na umri wa
miaka 81, Raha ya milele umpe Ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa
amani. Amina.