Kanisa litaendelea kutetea dhamana na utume wake katika sekta ya elimu
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda
na kiutetea dhamana na utume wake katika sekta ya elimu, ili kuwajengea wanafunzi
uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkubwa, huku wakizingatia
maadili na utu wema.
Kwa kutambua
dhamana hii, hapo tarehe 10 Mei 2014, Baraza la Maaskofu, Waamini, Wanafunzi, pamoja
na watu wenye mapenzi mema, wataungana na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kutetea umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya.
Lengo ni kulinda, kutetea na kuendeleza sekta ya elimu hasa wakati huu wa mtikisiko
wa uchumi kimataifa unaopelekea Serikali kubana matumizi hata katika Sekta ya Elimu
inayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na
Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wakati
alipokuwa anafafanua kuhsu utekelezaji wa mikakati ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia katika sekta ya elimu kwa kipindi cha Miaka kumi. Maaskofu wanasema kwamba,
elimu ni kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, malezi na majiundo ya binadamu ni
muhimu sana kabla ya kuweka mbele faida na masilahi ya mtu binafsi au kikundi cha
watu.
Shule ni mahali ambapo vijana wa kizazi kipya wanajenga na kudumisha
misingi ya kijamii, kiutu na kiakili, kumbe, umuhimu wa shule makini ni jambo ambalo
haliwezi kufumbiwa macho katika Jamii inayojikita katika maendeleo ya watu wake! Kanisa
katika mikakati yake ya kichungaji, daima limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee katika
sekta ya elimu kwa kutambua umuhimu wa elimu katika majiundo ya mtu mzima: kiroho
na kimwili; elimu inayomwezesha mwanadamu kuwa huru na mwenye ufahamu mpana katika
kuchambua na kunyambulisha mambo, ili kujenga na kudumisha Jamii inayosimikwa katika
ukweli, amani, haki na usawa.
Maaskofu wanatambua kwamba, athari za myumbo
wa uchumi kimataifa zimewatumbukiza wananchi wengi wa Italia katika umaskini wa hali
na kipato kiasi kwamba, kuna baadhi ya familia zinakosa mahitaji yake msingi, lakini
shule zinapaswa kuthaminiwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati
ya Serikali na wadau mbali mbali wa elimu nchini Italia. Hii ni sekta inayohitaji
Serikali kujisadaka, kwa ajili ya mafao na ustawi wa demokrasia. Kuna haja pia kuweka
uwiano mzuri kati ya kazi na elimu, ili kusaidia mchakato wa mabadiliko katika Jamii.
Askofu
Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, juhudi
zote hizi zinazofanywa na Kanisa Katoliki nchini Italia ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo
na mafao ya wengi.